BARA la Afrika linakabiliwa na changamoto nyingi katika kuleta mageuzi katika kilimo chake, lakini ni muhimu kama changamoto hizo zinaweza kutatuliwa kwa pamoja kati ya Serikali na Sekta Binafsi.
Rais Jakaya Kikwete aliyasema hayo juzi katika mkutano wa wadau wa Uchumi waliokutana mjini hapa alipokuwa anazungumzia mageuzi na changamoto za uchumi na fedha zinazoikabili dunia kwa sasa.
Katika Mada inayohusu mtazamo na mwelekeo mpya wa Kilimo na hatua zinazoweza kuchukuliwa, Rais Kikwete alisema, sekta ya kilimo barani Afrika inahitaji mageuzi makubwa ya kukifanya kiwe cha kisasa na chenye tija na hatimaye kuweza kuzalisha chakula kwa ajili ya matumizi ya watu wake na ziada kwa ajili ya kuuza nje ya bara hilo.
“Ukizungumzia mageuzi ya kilimo unazungumzia kilimo kinachotegemea sayansi na teknolojia ya kisasa itakayotufanya tutumie mbolea, mbegu bora, zana bora za kisasa ili kilimo hiki kiwe na tija,” alisema Rais na kuongeza kuwa, kwa kufanya hivyo, bara la Afrika litakuwa limewatoa wananchi wake kwenye umasikini mkubwa lakini pia kuongeza ajira na kuvutia maendeleo zaidi Barani Afrika.
Rais aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo unaojumuisha Viongozi wa Serikali, Wakuu wa Kampuni na Mashirika ya Kibiashara, Kifedha na Wataalamu mbalimbali wa Fedha na Uchumi duniani.
“Kilimo barani Afrika pia kimekuwa na changamoto nyingi kutokana na kuwa kinaendeshwa na Serikali, mara nyingi serikali zimekuwa zinakabiliwa na upungufu wa fedha hivyo kutenga fedha chache na zisizotosheleza katika kufanya shughuli za utafiti na kuboresha kilimo kwa ujumla,” Rais alisema na kutoa mwito kwa nchi tajiri, wafanyabiashara wakubwa na wadau wa maendeleo kutoa kipaumbele na kuanza kutilia maanani sekta hii ya kilimo barani Afrika.
“Tunaweza kushirikisha sekta binafsi ili kuchangia nguvu na mchango wa Serikali, kwa pamoja tutaweza kukuza kilimo cha Afrika na kukifanya kiwe na tija zaidi kwa wakulima na wadau wote kwa ujumla,” alisema na kutoa mfano wa mkakati wa kukuza kilimo Kusini mwa Tanzania unaohusisha mikoa mitano, iliyo katika ukanda wa Tazara maarufu kama Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT).
Alitoa mfano wa SAGCOT na kutoa changamoto kwa wadau na washiriki wa Mkutano wa mwaka huu wa Uchumi Duniani, maarufu kama World Economic Forum (WEF), kutumia mpango huu kama mfano wa kuigwa na kutumika katika nchi zingine za Afrika, ili kuboresha na kuleta mabadiliko katika kilimo barani Afrika na hatimaye, kuchangia katika kukuza uchumi na maendeleo ya bara la Afrika na dunia kwa ujumla.
Rais Kikwete aliondoka hapa jana kwenda Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria kikao cha kila mwaka cha Wakuu wa Nchi za Afrika.
0 Comments