WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema CCM katika mchakato wake maarufu wa kujivua gamba, haina budi kurudia zama za TANU na kupiga vita tabia inayoota ya kununua
madaraka wakati wa uchaguzi.

Pia ameitaka Serikali iachane na nyongeza ya posho za wabunge kutoka Sh 70,000 kwa siku mpaka Sh 200,000 kwa kuwa suala hilo linaweza kumweka pabaya hata Rais.

Sumaye alisema hayo kupitia kipindi cha televisheni ya ITV cha Dakika 45 kilichorushwa juzi usiku, alipokuwa akizungumzia mambo mbalimbali ya chama na Serikali kwa Tanzania na Afrika.

Kujivua gamba “CCM iliamua kwa nia njema kuwa kuna tatizo la rushwa na ufisadi na kuwataka waliokiingiza chama katika aibu ya kutumia rushwa wajiondoe wenyewe…tafsiri yake ni
magamba yajiondoe yenyewe,” alisema Sumaye.

Alisema kama kati ya waliotakiwa kujivua magamba katika ngazi tofauti za chama hicho wako waliokataa, kazi ya chama kwa sasa ni kuwashughulikia.

“Kama kuna gamba limeng’ang’ania, basi apatikane mtu wa kulivua kwa nyuma … CCM ina watu jasiri wa kuyatoa hayo makoti (magamba), tunajua yana fedha na dhahabu lakini yakitoka hayana nguvu,” alisema Sumaye.
Alifafanua kuwa kama mtu anatumia rushwa kupata cheo, akiondolewa katika hicho cheo,
maana yake hatakuwa na pa kumfanya atumie rushwa.



“Rushwa ni balaa katika uchaguzi, hatuwezi kuchaguana kwa rushwa, lazima turudi enzi za
TANU, hakukuwa na ‘bahasha’ katika uchaguzi,” alisema na kuongeza kuwa CCM haijapambana
vizuri na rushwa.

Alifafanua kauli hiyo kuwa katika mapambano ya rushwa, kumejitokeza kambi mbili; moja ya wanaojiita wapambanaji wa rushwa wanaodaiwa kutaka kuiondoa kambi nyingine katika
ushindani.

Alihoji kwa nini hiyo kambi inayopigwa vita haisimami hata siku moja na kusema inapiga vita
rushwa na badala yake jamii inashuhudia nguvu kubwa ikijaribu kunyamazisha wanaopambana na rushwa.

“Rais Kikwete (Jakaya), aliikuta rushwa na ataiacha, tunapaswa kuendelea kupambana na
wanaonunua madaraka, mtu akiingia serikalini kwa kununua madaraka, atatafuta fedha
kununua tena kwa bei ya juu na si kuhudumia wananchi.

“Hali ni mbaya na watu wakati wa uchaguzi wamefikia hatua ya kuita wakati wa mapato, kwa
namna hii Taifa litakwisha,” alionya na kuongeza kuwa watu wamechoka na kama CCM ikishindwa iseme na wananchi wataiondoa madarakani.

Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Tatu, alisema anatarajia
kazi ya kujivua gamba itafanikiwa na katika uchaguzi ujao wa ndani wa CCM utakaofanyika
mwaka huu, hakutakuwa na vitendo vya rushwa kama ambavyo imekuwa ikifanyika.

Posho na hatari kwa uongozi
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu nyongeza ya posho za wabunge, Sumaye alisema kwanza suala hilo halijaeleweka vizuri kwa kuwa kumejitokeza
kupingana kati ya Spika wa Bunge, Anne Makinda na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, huku Ikulu ikiwa kimya.

“Kama unataka kuwa mwanasiasa mzuri, unaposimamia kitu cha maslahi yako kinachokera
wananchi, ujue umekosea,” alisema Sumaye.

Hata hivyo alionya kuwa ikiwa Serikali itabariki nyongeza hiyo ya posho, kesho yake walimu nao watataka posho na baadae watafuata wanajeshi na ikifikia huko hata Rais wa nchi hatakuwa sehemu salama.

Alikumbusha kuwa baada ya miaka mitano ya kwanza ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, wakati wa kipindi cha pili alipotakiwa kuendelea kuwa Waziri Mkuu mwaka 2000, alikataa kwa kuwa alizuia nyongeza ya posho kwa wabunge.

“Nilimwambia Rais Mkapa, usinipe hicho cheo kwa kuwa kule bungeni hawanipendi nilizuia posho zao, akaniambia nenda nikakosa la kufanya,” alisema Sumaye.

Alionya kuwa suala la posho linapukutisha mapato ya Serikali kwa kuwa hata watumishi wa
umma wameamua kuhamishia makongamano mahotelini, kila kukicha kulipana posho na kusababisha mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kutoonekana yakifanya kazi.

Harakati za urais
Alipoulizwa kuhusu maneno yanayosemwa mitaani kuwa ana nia ya kugombea Urais wa
2015, Sumaye alisema hajaamua kufanya hivyo na siku akiamua, atatangaza.

“Urais lazima usubiri wakati ukifika ujipime kama unaweza na kama Watanzania wanakuhitaji
kwa nini usigombee?

“Kuwania urais si jambo baya hata ukitangaza leo, kwanza unaelezea mipango yako ya muda mrefu,” alisema na kuongeza kuwa haramu ni kutaka kumuondoa rais aliyepo madarakani au kupita pita kujaribu kufanya nchi isitawalike.

Umiliki wa mashamba Morogoro
Alipotakiwa kufafanua kuhusu mashamba anayomiliki Morogoro, kwamba anadaiwa alipora
wananchi ambao sasa hawana ardhi, alisema shamba hilo la hekta 300 halikuwa la wanakijiji.

Alifafanua kuwa shamba hilo, lilikuwa likimilikiwa na Chama cha Ushirika ambacho kililitoa
kama rehani ili kupata mkopo.

Kwa mujibu wa Sumaye, chama hicho kilishindwa kurejesha mkopo na mdai akataka
kulichukua, kikaona ili kuepuka hasara ni bora kuliuza.

“Sasa mimi kununua kitu kinachouzwa ni kosa?” Alihoji na kuongeza kuwa hata madai
kuwa ameliacha pori si ya kweli kwa kuwa kuna majani ya mifugo ambayo wanaoyaona wanadhani ni pori wakati hayatoshi kulisha mifugo yake.