Sehemu ya nyama inayopodaiwa kuwindwa na majangili kitalu cha Gonabisi Wilaya ya Morogoro, ikipakiwa kwenye gari

Venance George, Morogoro
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Ezekiel Maige na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, wametakiwa kuingilia kati kitendo kinachodaiwa kufanywa na Mwenyekiti Hifadhi ya Jumuiya ya Kuhifadhi Maliasili na Ukutu (JUKUMU), kwa kudaiwa kushirikiana na majangili kupiga wanyama katika kitalu cha Gonabisi, Wilaya ya Morogoro.

JUKUMU ni moja ya hifadhi 16 ilizobarikiwa kuwa na maliasili mbalimbali, ikiwamo wanyama na mimea inajumuisha vijiji 21 vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini.
Mmoja wa wanachama hao kutoka Kijiji cha Dutumu ,Issa Ally, alidai licha ya jitihada mbalimbali za kumuonya mwenyekiti wao kuacha kujihusisha na vitendo vya kushirikiana na majangili, hazijafanikiwa.

“Tumeshamfuata mara kadhaa baada ya kusikia anashirikiana na majangili achane na vitendo hivyo, amekuwa akikataa kujihusisha navyo, hivyo tukaweka mkakati wa kupata ushahidi wa kumpiga picha akiwa anashiriki ndiyo hizi tunazo,” alidai Ally.
Inadaiwa mpaka sasa mwenyekiti huyo kwa kushirikiana na majangili hao ameshauwa nyati 16, pofu 11, swala 52, nyumbu 41 na kongoni 22 ambao inadaiwa amekuwa akishirikiana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Morogoro kumkingia kifua.
Naye Omari Selemani, kutoka Kijiji cha Magogoni, alidai vitendo vya ujangili vimekuwa vikipewa nafasi na baadhi ya viongozi wa Serikali na kwamba, waliwahi kumsimamisha uongozi mwaka 2008, lakini serikali ya wilaya ilimrejesha madarakani.

Kwa upande wake, Ofisa Wanyamapori Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa, alisema amekuwa akisikia taarifa hizo lakini ofisi yake haijapelekewa malalamiko hayo kwa maandishi na ushahidi, ili aweze kuchukuliwa hatua kutokana na vitendo hivyo.

“ Mimi sifanyi kazi kwa maneno kama wana ushahidi wa kutosha walete kimaandishi, tuweze kuchukua hatua zinazostahiki, “ alisema Chuwa kwa simu.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alipotafutwa kwa simu kujibu tuhuma hizo, baada ya kuelezwa madai hayo alikata simu hiyo na hata baadaye alipopigiwa simu hiyo hakuipokea. chanzo cha habari ni hapa.