Wahamiaji Haramu raia wa Ethiopia wakitelemka eneo la Mahakamani leo kutoka kwenye Lori lililowabeba wakisafiri kwenda nchini Afrika Kusini mara baada ya kukamatwa Mwishoni mwa wiki.
Wahamiaji haramu wa Raia wa Ethiopia wakiwa ndani ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro wakisubiri kusomewa mashitaka yao.

Habari na Picha na John Nditi, Morogoro

WAHAMIAJI haramu 98 wa kutoka nchini Ethiopia, pamoja na Watanzania wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Morogoro wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali,ikiwemo ya wahamiaji hao kuingia nchini bila kuwa na hati za kusafiria wala kibali kutoka Mamkala za Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Watanzania waliofikishwa Mahakamani hapo jana na kusomewa mashita yao ni Emili Kimario (33) mkazi wa Rombo, Mkoani Kilimanjaro ambaye ni Dereva wa Lori aina ya Fuso lenye namba za usajili T 718 AZY mali ya Emmanuel Juma ,pamoja na msaidizi wake , John Kisima (28) mkazi wa Himo, Mkoani Kilimanjaro ambaye ni ndugu mwenye Lori hilo.

Akisoma mashitaka mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Evodia Kyaruzi, Mwendesha Mashitaka wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Morogoro,Helmina Foya, akidai kuwa washitajiwa hao wawili ambao ni Watanzania wanathumiwa kuwasaidia raia wa Ethiopia 98 kuingia nchini bila kuwa na nyaraka halali pamoja na hati za kusafiria.

Pia alidai kuwa mnamo Januari 19, mwaka huu majira ya saa moja usiku eneo la Melela , Wilaya ya Mvomero , Mkoani Morogoro kuwa wakiwa ni madereva wa Lori la mizigo waliwabeba raia wa Ethiopia na kuwasafirisha wakati wao wakiwa hawana vibali wala hati za kusagiria sambamba na kutumia gari la mizigo kubeba abiria raiaa wa kigeni na kuwaingiza nchini.

Kwa upande wake Hakimu wa Mahakama hiyo, Kyaruzi, alipowata wajibu tuhuma hizo, kwa nyakati tofauti walikana kuhusika na kosa hilo , hata hivyo Mwendesha Mashitaka wa Idara hiyo aliiomba Mahakama kutotoa dhamana kwa watuhumiwa kufuatia kuonekana ni wazoefu wa usafirishaji wa Wahamiaji haramu.

Mwendesha Mashikata huyo alidai kuwa Watanzania hao walikamatwa miezi miwili iliyopita ( Mwaka jana) wakiwasafirisha wahamiaji haramu raia wa Ethiopia wapatao 103 kwa kutumia Lori hilo na baada ya kupigwa faini kwa mara nyingine limetumika kusafirisha wengine.

Hata hivyo Hakimu wa Mahakama hiyo alizingatia hoja ya upande wa Mashitaka kwa kukubaliana na hoja hiyo na kuzuia kutoa dhamana kwa watuhumiwa hao hadi suala hilo litakapokamilika.

Kwa upande wa kesi ya Wahamiaji hao haramu wa kutoka Ethiopia, Mwendesha Mashitaka huyo wa Idara ya Uhamiaji, aliomba mbele ya Hakimu kuisogeza mbele ili kutoa muda wa kumpata mkalimali wa kutafasiri lugha ya kihabeshi kwenda kiingereza na kiingereza kwenda kihabeshi kwa vile walikuwa hawafahamu lugha ya kiingereza.

Hata hivyo Hakimu wa Mahakama hiyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Februari 8, mwaka huu itakapotajwa tena sambamba na watanzania hao wawili , hivyo wote kurudishwa rumande hadi siku hiyo.