SIKU mbili baada ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) sehemu ya Mlimani, kuwatimua wanafunzi 13 na Baraza la Chuo kubariki hatua hiyo, wengine watatu wamekamatwa na polisi kwa kuwavurugia mitihani ya majaribio wenzao zaidi ya 150, jana asubuhi.

Aidha, Baraza hilo lililokutana kwa dharura juzi mchana na kubariki uamuzi huo, limesisitiza kuwa timuatimua haitakoma kwa mwanafunzi atakayejihusha na uvunjaji wa sheria na taratibu za chuo hicho, hadi nidhamu itakaposhika mkondo wake.

Akizungumza Dar es Salaam jana kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Udsm, Profesa Rwekaza Mukandala, Mkuu wa Taaluma chuoni hapo, Profesa Makenya Maboko, alisema vitendo vya ukiukaji wa sheria na taratibu miongoni mwa baadhi ya wanafunzi vimeendelea kukiathiri.

Alisema vitendo hivyo vimefikia hatua mbaya, kiasi cha wanafunzi wachache sasa kuthubutu kuwachapa wenzao wanaoendelea na mitihani ya majaribio ili waisusie.

Kwa mujibu wa Profesa Maboko, licha ya chuo hicho kuchukua hatua ya kuwafukuza vinara wa mgomo na fujo za Januari 09, wanafunzi wengine watatu waliwavamia wenzao zaidi ya
150 katika vyumba vya majaribio ya mitihani jana asubuhi, kuwachapa na kuwavurugia mitihani.


“Ndiyo maana askari wa kulinda amani wako hapa muda wote, wamekamata wanafunzi hao watatu (hakuwataja) na kuwapeleka Kituo cha Polisi Oysterbay ili hatua zaidi za kisheria zichukue nafasi yake. “Kuna madai kuwa ni miongoni mwa waliofukuzwa, lakini uhakika
zaidi utapatikana kadri taarifa sahihi zinavyotufikia,” alisema.

Alionya, kuwa kitendo hicho ni batili na hakuna jinsi ya kukivumilia, na ndiyo maana Baraza likatoa msimamo kuwa wote watakaojihusisha na uvunjaji wa sheria wachukuliwe hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwafukuza.

”Tunachukua hatua ya kuwasimamisha au kuwafukuza, baada ya kujiridhisha kuwa wanastahili
adhabu husika,” alisema Profesa Maboko.

Fukuza hiyo iligusa baadhi ya mawaziri na wabunge wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) waliodaiwa kuponzwa na hoja binafsi iliyotolewa na mmoja wa wabunge wa Baraza la Wanafunzi, na kuibua suala la kufukuzwa kwa wenzao 48 Desemba
14.

Kwa maelezo ya Profesa Maboko, hoja hiyo iliwataka wabunge wapige kura kupitisha mgomo wa wanafunzi ambao hata hivyo, ulibarikiwa na baadhi ya viongozi wa Daruso.

“Walichokifanya ni batili na hoja iliyoleta matatizo haya ilitolewa wakati nusu ya wabunge wakiwa wamekwishatoka nje ya ukumbi, baada ya ajenda mbili za siku hiyo kujadiliwa.

Kati ya wabunge waliobaki ukumbini, watano ndio walipiga kura ya kukataa mgomo wakati 56
waliukubali huku wakijua si sahihi. “Lakini haki imetendeka na itaendelea kutendwa, huku Daruso kama Serikali ya Wanafunzi ikiendelea kutambuliwa na chuo, kuwa ni halali.
Haihukumiwi kama chombo na wala haitafutwa, kwa sababu ya kilichotokea, bali mwanafunzi mmoja mmoja ndiye ataguswa kulingana na makosa yake,” alifafanua.

Wanafunzi 85 akiwamo Rais wa Daruso walisimamishwa kwa muda usiojulikana katika tukio la Jumatatu wakati wanne walisimamishwa kutokana na tukio la mwishoni mwa mwaka jana.

Miongoni mwa waliofukuzwa na kukabidhiwa barua zao juzi ni Spika wa Bunge la Wanafunzi, Peter Anold na mawaziri wa Daruso; Naftal Daniel (Mikopo) Mwakyusa Daniel na Naibu wake Masiga Gulatone (Taaluma).

Wamo pia viongozi wengine tisa wa Serikali hiyo pamoja na Wilfred Bocasa wa mwaka wa pili asiye na wadhifa.