Maelfu ya watu wakiwa kwenye sherehe za kilele cha Maadhimisho ya Miaka 35 ya Kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza jana. Katika sherehe hizo, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete alihutubia. (Na Mpiga picha Maalumu)
CCM IMEWABEEP WAPINZANI.
NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ‘kimewabeep’ wapinzani kwa kufanikisha maadhimisho ya miaka 35 tangu kuanzishwa kwa chama hicho 05/02 mwaka 1977.
Ndugai amesema, kufana kwa maadhimisho hayo ina maana kwamba, wapinzani waiachie njia CCM iendelee kutawala.
“Uwanja wa Kirumba ulijaa, ukafurika, ukatapika mpaka nje…hii maana yake ni kwamba, tumebeep, tunahitaji njia kwa watani wetu” amesema Ndugai kabla ya kuahirisha kikao cha Bunge mjini Dodoma.
Kwa niaba ya Bunge amekipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kufikisha miaka 35 tangu kuanzishwa kwake.
Wabunge wengi hususan wa CCM walionekana kuiunga mkono kauli ya Ndugai kwa kugonga meza.
“Wengine mbona hampigi makofi, hii ni birthday party tu” alisema Ndugai.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete jana aliongoza maelfu ya wananchi katika kilele cha sherehe za kutimiza miaka 35 ya CCM kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Katika maadhimisho hayo Kikwete alisema, viongozi na wanachama wasiotaka mabadiliko ndani ya chama hicho , hawakitakii mema chama hicho na kama wanadhani uamuzi huo ni wa hovyo, basi wao ndiyo wa hovyo.
“Chama chetu ni cha siku nyingi jambo ambalo lina faida na hasara zake. Kwa sababu ya kujulikana sana na uzoefu wake kinaweza kuwa na fursa ya kupata ushindi hasa pale ambapo watu wameridhika na matendo yake au wana hofu na mabadiliko.
“Kwa sababu hiyo, CCM lazima wakati wote ibaki kuwe Chama cha matumaini ya mambo mapya mazuri kwa wananchi. Kitoe matumaini ya kuwa Chama cha kuleta mabadiliko yenye tija na Chama kinachotenda mema.
“Kwa maneno mengine, Chama Cha Mapinduzi kiige tabia ya nyoka ya kila baada ya muda fulani hujivua gamba lake na kupata jipya. Hatuna budi kufanya hivyo na kufanya hivyo sasa,” alisema Rais Kikwete mwaka jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Lakini mageuzi hayo yamepokewa kwa mitazamo tofauti ndani ya chama hicho na baadhi ya viongozi na wanachama wake kuyapinga na kuyapa dhana tofauti, ili yaonekana kama yana lengo la kufukuza baadhi ya wanachama wanaotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali ndani ya chama na nje ya chama hicho tawala.
Rais Kikwete alisema anatambua kilio cha wanachama na wananchi cha kutaka CCM iwe na viongozi waadilifu na sio wenye tuhuma za mambo ya hovyo.
“Kilio hiki kinaonesha wengi wana imani na CCM, wanataka tukisafishe, wangekuwa wamekichoka wangekaa kimya wasubiri kutunyima kura katika uchaguzi…tusichelee kuwaudhi wanachama wachache kwa maslahi ya wengi,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa kazi hiyo ataifanya mpaka ifikie ukomo.
Kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama, Rais Kikwete alisema walikubaliana uchaguzi wa ndani ya chama na jumuiya zake ufanyike katika mwaka mmoja, ili chama kiwe na miaka minne ya kujijenga na kujiimarisha.
Aliwataka wanachama hao kutumia fursa ya uchaguzi mwaka huu kupata viongozi watakaojenga chama, wabunifu na wenye uwezo wa kutetea sera za CCM.
“Sio mchague viongozi wasio na mbele wala nyuma… viongozi wanapaswa kuwa chemichem ya mawazo, tusichague wenye upeo mfupi ambaye wakati mwingine unatamani asifungue mdomo, akifungua anasema sivyo mnaachiwa kazi ya kusafisha,” alisema mwenyekiti huyo wa Taifa wa CCM.
“Tusichague viongozi wanaotaka kujinufaisha wenyewe badala ya Chama na kusababisha jamii wagune kutokana na tabia zao mbaya zisizo na uadilifu kwenye jamii kwani viongozi wasio na sifa njema huathiri hadhi ya Chama,” alisema Kikwete.
“CCM iachane na viongozi wasio na sifa njema, wachochezi, waongo, wala rushwa, wenye majungu, wabaguzi na wasio waadilifu, mnawajua kwa kauli na matendo yao, timizeni wajibu wenu kupitia uchaguzi wa Chama,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa ndio maana kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema ‘CCM imara inaanza na mimi’.
Huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliofurika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Rais Kikwete alisema CCM si chama cha kifalme na mtaji wake ni watu na kutaka nguvu ya chama ielekezwe kwenye matawi tofauti na awali ambapo zilielekezwa kwenye wilaya na mikoa.
Alisema wapo viongozi wengi hawana uhusiano na walio katika ngazi za chini kwa kusema wao ni wa taifa, wanatakiwa kujua kuwa kazi yao ni kuimarisha Chama kuanzia kwenye matawi na kuongeza kuwa anayetaka ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa aende wilayani.
Rais Kikwete alisema CCM ndio mlezi wa Taifa la Tanzania na kunukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa ‘Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba.
“Nawasihi tutumie vizuri chaguzi hii kupata viongozi bora wasio kigawa Chama na wenye uwezo wa kukisemea,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa sifa ya uongozi kununuliwa imekivunjia heshima Chama hicho kwa jamii ndio maana katika Sheria ya Uchaguzi na uchaguzi wa vyama vya siasa ukawekwa.
Aidha, Rais Kikwete aliwataka wana CCM hasa vijana na wanawake kujitokeza kugombea nafasi za chama na kuhoji kama vijana hawatapewa uongozi, CCM itaachwa kwa nani.
0 Comments