Na Waandishi Wetu
BIFU la chinichini lililopo kati ya Wema Isaac Sepetu na Kajala Masanja linadaiwa kusababishwa na kuchanganywa kwao kimapenzi na ‘brazameni’ wa Bongo Fleva na filamu, Hemedy Suleiman ‘PHD’ chanzo kina muvi kamili.Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika, vuguvugu la ugomvi kati ya wawili hao limetokana na wivu wa kimapenzi kati yao na staa huyo aliyewahi kutamba katika Shindano la Project Fame nchini Kenya.
Inadawa kuwa, mastaa hao wa kike, kila mmoja kwa wakati wake ameshatoka na Hemedy kimapenzi, hivyo wanachokifanya sasa ni kuoneshana ubabe kama siyo kutambiana na kuoneshana jeuri.
Awali, Hemedy alikuwa akitoka na Kajala lakini katika hali ya kutatanisha kukatokea kutokuelewana kati yao ndipo alipoamua kuwa ‘so klozi’ na Wema ambaye awali alikuwa akimwita shemeji.
Gazeti hili limebaini kuwa Wema amekuwa akimtesa Kajala kwa kuweka picha alizopiga na Hemedy katika kurasa za mtandao maarufu wa BBM ambao unatumiwa na watu wenye simu aina ya Blackberry tu.
Kitendo hicho cha Wema kimekuwa kikimuumiza Kajala na kumfanya kulalamika kwa baadhi ya marafiki zake.
Risasi Jumamosi, baada ya kupata habari hizo za ndani, lilimtafuta Hemedy ili kusikia utetezi wake juu ya madai hayo yanayomkabili.
“Kwa kweli Wema ni rafiki yangu wa kawaida tu, hizo picha anazoziweka BBM nazitambua, hata mimi nimekuwa nikiziweka, nilipiga naye siku ya Valentine’s Day pale Bilicanas, nilipokuwa kwenye shoo,” alisema Hemedy.
Hata hivyo, pamoja na kukataa ‘kudeti’ na Wema, habari chini ya kapeti zinasema kuwa staa huyo mtanashati anazuga tu ili asipangwe kwenye mnyororo wa mastaa waliowahi kutoka na mlimbwende huyo wa mwaka 2006.Kuhusu suala la kuwagombanisha Wema na Kajala, Hemedy alisema wala hafahamu kama wanagombana kwa sababu yake.
“Kajala alikuwa mpenzi wangu, ila tulishaachana kitambo sana, sasa sijui kama anagombana na Wema kwa sababu yangu,” alisema Hemedy kwa kifupi.
Kajala alizungumza na gazeti hili hakukataa wala kukubali juu ya kutoka na Hemedy, alisema picha za Wema na Hemedy amekuwa akiziona kwenye mtandao wa BBM na wala hazimshtui.
“Binafsi wala sielewi wanamaanisha nini kwa kuziweka picha hizo, hata hivyo sitaki kuongea sana kwa sababu sielewi kitu zaidi ya kuziona picha hizo tu,” alisema Kajala.
Jitihada za kumsaka Wema hazikuzaa matunda kwani alipotafutwa kwa kupigiwa simu, ilikuwa ikiita bila ya kupokelewa.

Habari hii imeandikwa na Musa Mateja, Imelda Mtema na Gladness Malya.