ASEMA YANAYOFANYWA NA POLISI YATASABABISHA NCHI ISITAWALIKEGeofrey Nyang’oro
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ameionya Serikali ya Jakaya Kikwete kuwa mambo mbalimbali yanayoendelea kutokea nchini, likiwemo tukio la hivi karibuni la polisi kuua raia wanne kwa risasi mjini Songea, yanaweza kuifanya nchi isitawalike.Akizungumza katika uzinduzi wa jengo la vijana wa chama hicho (Bavicha) lililopo Kinondoni jijini Dar es Salaam jana, Dk Slaa alisema kamwe wananchi hawawezi kuvumilia kitendo cha polisi kuua raia wasio na hatia.

“Nimewahi kutoa kauli kuwa nchi haitatawalika, sikuwa na maana kuwa Chadema itaongoza harakati za kupinga nchi isitawalike, bali vitendo vya viongozi na watendaji wa Serikali kukiuka sheria wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ndio kunaweza kuifanya nchi isitawalike,” Dk Slaa alisema mauaji ya Songea ni matokeo ya viongozi wa mkoa huo kushindwa kusoma saikolojia ya wananchi walipoandamana wakipinga wenzao kuuliwa katika mazingira ya kutatanisha.

Alisema kitendo cha viongozi hao kushindwa kusoma saikolojia ya wananchi hao na kukataa kuwasikiliza huku wakiamuru polisi kuwatawanya ndio kilichosababisha watu wasio na hatia kupoteza maisha. Alisema katika mazingira hayo, Serikali inapoteza uhalali wa kuwatumikia wananchi kwa sababu polisi wanaotakiwa kulinda usalama wa raia, wanafanya mauaji huku viongozi waliopewa jukumu la kuwalinda, wakibariki vitendo hivyo. Dk Slaa alimtaka Rais Kikwete kuwavua nyadhifa viongozi wakuu wa mkoa huo na kuunda tume huru ya kuchunguza chanzo cha mauaji hayo.

“Tukio la Songea linasikitisha sana, namshauri Rais Kikwete awaondoe kwenye nyadhifa zao Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kupisha uchunguzi wa mauaji hayo, pia tume zilizoundwa na viongozi hao wa mkoa, zivunjwe sababu hazina tija, tunahitaji tume huru Songea,” alisisitiza Dk Slaa. Dk Slaa alisema chama chake hakiwezi kukubali kuona haki za binadamu zikikiukwa na kwamba, kitashughulikia tukio la Songea kuhakikisha kuwa ukweli unapatikana

na wahusika wanachukuliwa hatua. Katika kutekeleza hilo, Dk Slaa ametoa wiki mbili kwa Bavicha kufuatilia na kukabidhi ripoti ndani ya wiki mbili, ili chama hicho kiweze kuchukua hatua.

Kushushwa bendera za Chadema
Akizungumza suala la madai ya kushushwa bendera za chama hicho alilodai liliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduma, Dk Slaa alisema kuwa vitendo hivyo vinachochea vurugu nchini. “Juzi nilipigiwa simu na kuambia Mkuu wa Wilaya akiongozana na Kamanda wa Polisi, wameshusha bendera za Chadema…, inapofikia hatua Mkuu wa Wilaya anaongoza harakati za kushusha bendera ili Makamu wa Rais aweze kufanya ziara eneo husika, ni kuchochea vurugu,” alisema Dk Slaa Alisema baada ya kupata taarifa hizo alimpigia simu Mkuu huyo wa Wilaya kumuuliza na baadaye akamuuliza Mkuu wa Mkoa huo, Abass Kandoro aliyetaka amueleze kama katika katiba ya nchi Chadema haitakiwi kuwa katika mkoa wa Mbeya.

Amvaa Tendwa Dk Slaa pia alimvaa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini,
John Tendwa kuwa kitendo chake cha kudai Mbunge wa Arusha Mjini Godles Lema hatakiwi kufika katika Jimbo la Arumeru Mashariki, ni sawa na kufanya kampeni za kisiasa za kukitafutia ushindi CCM. Awasihi vijana Mara baada ya kuzindua jengo hilo la vijana, aliutaka uongozi wa vijana hao ukiongozwa na Mwenyekiti wake, John Heche kutumia fursa ya kuwa na jengo lao kuunganisha makundi ya vijana wa aina mbalimbali ili kuleta ukombozi katika Taifa.


Alisema kwa sasa vijana wamegawanyika katika makundi mbalimbali kwa misingi ya itikadi za kisiasa, lakini akawataka viongozi hao kuwaunganisha kwa pamoja. Kwa upande wake, Heche alisema wao kama vijana watalitumia jengo hilo kuongoza harakati za kuleta mageuzi nchini ili kuwezesha Watanzania kujikomboa.