Waandishi Wetu
MGOMO wa madaktari nchini umeingia katika sura mpya baada ya wanaharakati kutoka asasi 15 za kiraia kufanya maandamano ya amani jana, wakitokea maeneo mbalimbali kuelekea Ikulu jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuwasilisha kilio chao kwa Rais Jakaya Kikwete. Hata hivyo, wanaharakati hao hawakufanikisha lengo lao baada ya kujikuta wakidhibitiwa na kusambaratishwa na polisi waliokuwa na silaha .


Pamoja na kukwamishwa mkakati wao huo, wameipa Serikali saa 24 kuchukua hatua za haraka kumaliza mgomo wa madaktari na kutishia kwamba kinyume na hapo, watawahamasisha wananchi kuingia barabarani, kufanya maandamano makubwa ya kuishinikiza Serikali kujiuzulu.

Kwa muda wa wiki mbili sasa nchi imekuwa ikitikiswa na mgomo wa kihistoria wa madaktari, ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa utoaji huduma za afya kwenye hospitali za rufaa ikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa (MOI), ambako huduma zimesitishwa.

Katika maandamano ya jana, wanaharakati hao walifunga Barabara za Ali Hassan Mwinyi na Ocean Road kwa muda wa saa moja na kusababisha foleni kubwa ya magari.

Maandamano hayo ya kushtukiza yaliyoanza saa 8:00 mchana, yalishirikisha asasi za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa).


Awali, wanarahakati hao walianza kujikusanya taratibu kati ya eneo la Hoteli ya Palm Beach na Kituo cha Polisi cha Oysterbay kilichopo jirani na daraja la Salender, huku wengine wakilala barabarani.

Wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, wanaharakati hao wametaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na Naibu wake, Lucy Nkya na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni wajiuzulu kwa kuwa wanafanya mzaha kwasababu Rais na viongozi wengine hawatibiwi nchini wakiugua. Katika maandamano hayo, waanaharakati hao pia walimlaani Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa kuzuia kujadiliwa kwa suala hilo la dharura na kuongeza kwamba, kwa kuwa tatizo linajulikana hakukuwa na haja ya kuunda kamati kutafuta chanzo.

Akizungumza jana Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya alisisitiza kuwa maandamano hayo ni ya wananchi. Alieleza kuwa ujumbe wao walioutuma kwa Serikali usipotekelezwa, watawaambia wananchi waingie mtaani kudai haki yao ya kupata matibabu.

“Tunatoa saa 24 kwa hatua za haraka kuchukuliwa kuhusu mgomo wa madaktari la sivyo, kesho (leo) tutawaeleza wananchi jinsi ya kuingia barabarani ili kuishinikiza Serikali ijiuzulu,”alisema Nkya.

Mratibu wa Mtandao wa Asasi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani Arusha (Angonet), John Bayo, alisema mgomo wa madaktari unapaswa kusitishwa sasa, kwa pande hizo mbili yaani Serikali na madaktari, kukaa na kukubaliana.

“Lazima wakae, watu wanakufa kwa kukosa matibabu, hapa hatafutwi mshindi bali haki na maisha ya watu,”alisema Bayo. Bayo alisema katika kikao hicho kwa kuwa madai ya madaktari yanafanana na wafanyakazi wengine wa umma katika sekta nyingine, lazima kuwapo mpango wa kumaliza matatizo ya muda mfupi, wa kati na mrefu.

Alisema haiwezekani sasa maisha ya watu yanapotea, huku Bunge likiendelea kulumbana na Serikali ambayo nayo inatoa matamshi ya vitisho kwa madaktari jambo ambalo, si jema.

Polisi
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alisema watu hao walikuwa wamekusanyika eneo la Palm Beach na kwamba, mkusanyiko huo ulilenga kuwashawishi madaktari kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa. “Lilikuwa kundi la watu takribani 150 na walikuwa wakitaka kufanya maandamano kushinikiza madaktari kurudi kazini…, tulichokifanya Polisi ni kuwataka watawanyike na walitii amri hiyo,” alisema Shilogile.

Alisema kazi ya Jeshi hilo sio kutatua tatizo la mgomo wa madaktari bali ni kuhakikisha usalama wa raia na kwamba, watu hao wanatakiwa kuwasilisha madai yao sehemu husika.

Bungeni

Mgomo huo jana ulirindima tena bungeni baada ya kipindi cha maswali na majibu, kufuatia Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), akiwa ni mbunge wa sita kutaka kujadiliwa hoja hiyo, aliomba kwa kutumia kanuni ya 47, Bunge kujadili jambo hilo la dharura. “Naibu Spika, nchi yetu inalo jambo la dharura sana. Hii ni karibu wiki ya pili Watanzania wenzetu wanakufa mahospitalini. Hili limekuwa linaombwa hapa, naona tena leo niombe Bunge lako lijadili suala la mgomo wa madaktari pamoja na yote yanayoendelea. Wako watu wanaosema ni kuingilia mihimili mingine, hapana, wanaokufa ni Watanzania ambao leo tuko hapa kuwawakilisha,” alisema Serukamba na kuongeza:

“Litakuwa Bunge la ajabu sana na tutaingia kwenye historia, Watanzania wanakufa tunasema hatuwezi kuingilia mhimili mwingine. Ninaomba leo wabunge mniunge mkono ili Spika uamue sasa tuanze kujadili suala hili gumu ambalo Watanzania wanapoteza maisha yao.” Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na kukubaliwa na wabunge wote. Lakini, akitoa mwongozo wake, Naibu Spika Job Ndugai, alisema kwa mujibu wa Ibara 63 ya Katiba ya Nchi, inatambua Bunge kama chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambacho kitakuwa na madaraka ya niaba ya wananchi kusimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote.

“Sasa huwezi kusimamia jambo au huwezi kuwa mshauri mzuri kama hujapata ukweli au hujapata kidogo undani wa mambo na ndiyo maana jambo hili mliposimama mara ya kwanza, tena mkasimama tukashauri kwamba ni vizuri liende katika Kamati yetu ili tutakapoishauri Serikali, tukiwashauri hawa watumishi wa Serikali tuwe tunatoa ushauri ambao unatokana na watu ambao wako informed,(wanauelewa)” alisema Ndugai. Madaktari Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari inayosimamia madai yao Dk Stephen Ulimboka, alisema lawama zinazotokana na wagonjwa kwa kukosa tiba zinapaswa kuelekezwa serikalini.

Dk Ulimboka alitoa kauli hiyo jana alipotakiwa kuelezea hataua walizofikia kati yao na Serikali kuhusu mgomo unaoendelea hivi sasa. “Tangu madaktari wagome leo (jana) ni siku ya 16, Kamati iliyoundwa na Serikali kushughulikia suala hilo haijawahi kutoa taarifa yoyote wala kukutana nasi, sisi tulishasema na leo tunarudia, milango iko wazi kwa ajili ya majadiliano na Serikali,”alifafanua Dk Ulimboka.

Alisema kimsingi, wao wanaumizwa na hatua hizo, lakini, akadai msimamo wao unadai haki zao sababu wamelenga kusaidia haki zao na za wananchi ambao wanakosa tiba bora kutokana na Serikali kutozingatia umuhimu wa huduma za afya hapa nchini.

Dk Ulimboka alisema kamati yake imeendelea na vikao kujadili mambo mbalimbali huku ikisubiri tamko litakaloonyesha nia ya Serikali ya kushughulikia madai yao.

Viongozi wa dini

Katibu wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Arusha, Abbas Mkindi maarufu kama Darwesh, alisema baraza hilo linapinga mgomo, lakini pia linataka Serikali kukaa na madaktari.

“Lazima Serika imalize mgogoro huu na pia ichunguze chanzo chake na hizi kauli za watendaji wake, kwani hapa tunahisi kuna hujuma dhidi ya Serikali ya Rais Kikwete, ”alisema Mkindi. Kwa upande wa Mchungaji Anicet Maganya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Arusha, alisema kubwa katika madai ya madaktari ni maslahi, lakini wameonekana kukerwa na majibu ya watendaji wa Serikali na vitisho. Mchungaji Maganya ambaye ni Mkuu wa Idara Utetezi ya Kanisa hilo , alisema ingawa haungi mkono mgomo unaoendelea anaamini kauli za viongozi wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwatisha madaktari ndio umefikisha hapa.


Habari hii imeandaliwa na Geofrey Nyang’oro, Joseph Zablon, Dar na Mussa Juma, Arusha