Marekakani imesema kuwa mataifa ya kirafiki yanayoitakia Syria utawala wa Kidemokrasia yanapaswa kuungana katika kumshutumu kiongozi wa taifa hilo Rais Assad.
Waziri wa mashauri ya Kigeni wa Marekani, Bi Hillary Clinton, alisema ni jambo la kusikitisha kuwa Urusi na Uchina zilipiga kura za turufu kupinga azimio la kuikosoa Syria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Alitoa wito kwa jamii ya kimataifa iunge mkono makundi ya upinzani nchini Syria.
Ni wazi kwamba Marekani pamoja na wanadiplomasia wa mataifa mengine ya Magharibi wameghadhabishwa mno na hatua ya Urusi na Uchina kupinga azimio la kuikosoa Syria.
Bi Clinton alikuwa akizungumza akiwa Bulgaria ambako amesema Marekani pamoja na mataifa mengine zitashinikiza rais Assad aondoke mamlakani.
Alizungumzia kuhusu kuwekwa vikwazo zaidi pamoja na kuwataja watu ambao wanafadhili na kuipa silaha serikali ya Syria.