HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, imeamua kufuatilia ushuru wake wa Sh milioni 36 kwa kila mwezi kutoka kampuni ya Pan African Energy na Shirika la Taifa la Maendeleo ya Mafuta (TPDC) kutokana na kuzalisha gesi ya Songosongo, mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Steven Mapunda alisema hayo juzi wakati akizungumza na wachimbaji na wamiliki wa migodi midogo na kuongeza kuwa ushuru wa mamilioni ya fedha unapotea huku mamlaka ikiwa masikini.

Alisema ilishachukua hatua kadhaa pamoja na kuwaandikia barua ili kukamilisha utaratibu na kuanza kulipwa ushuru huo, kutokana na gesi inayozalishwa katika Kijiji cha Songosongo , wilayani Kilwa. Kwa mujibu wa Mapunda, mashirika hayo kwa pamoja wanauzia umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kupata Sh bilioni 12 kwa kila mwezi, kwa hiyo halmashauri nayo inatakiwa ipatiwe mgawo wake wa Sh milioni 36.
Mapunda alisema halmashuri hiyo vile vile inafuatilia kwa karibu ushuru wa madini ya jasi yanayopatikana katika vijiji vya Makangaga, Mandawa na Kiranje ranje. Alisema kuanzia sasa wachimbaji wa madini hayo walishakubaliana kila tani moja, ushuru wa halmashauri utakuwa Sh 1,000 na lori lenye ujazo wa tani 20 watalipa Sh 20,000.

Mapunda alisema fedha nyingi za halmashauri zinapotea kutokana na usimamizi wa makusanyo ya ushuru kuwa hafifu kutoka kwa watendaji na wamiliki wa migodi hiyo. Alisema ushuru mwingine unaopotea ni pamoja na wa uvuvi wa samaki wabichi na wakavu na pweza kwa kuwa fedha zinazopatikana ni tofauti na idadi inayosafirishwa kutoka katika mkoa huo.

Alionya endapo itatokea uzembe wa ukusanyaji utakaobainika kwa watendaji, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao. Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ilianzishwa mwaka 1948 lakini mpaka leo ni masikini kuliko Halmashauri ya Nanyumbu ambayo iko juu kiuchumi pamoja na kuwa mpya.

Kamishina Msaidizi wa Madini kutoka Wizara ya Nishati na Madini Kanda ya Kusini, Aloyce Tesha alisema halmashauri zinatakiwa kuunda sheria ndogo ili zipate kukusanya ushuru wake wa madini.


                                                                          Toka Habari Leo.