MALABO, Guinea
MASHABIKI wa timu ya taifa ya Ivory Coast wamemtungia wimbo maalum mama mzazi wa nahodha wao, Didier Drogba, ikiwa ni sehemu ya kumshukuru kutokana na chakula anachowapikia.
Clotilde Drogba amekuwa akiwapikia chakula cha bure mashabiki zaidi ya 60 walio mjini hapa ili wapate nguvu ya kuishangilia timu yao inayoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika. Leo inacheza nusu fainali dhidi ya Mali.
Mama huyo wa Drogba amekuwa akipika msosi wa asili kama kuku, ‘mchele’ ili kuwafanya mashabiki hao waone kama wako nyumbani. Hakuna anayelipa, badala yake mashabiki hao hupata chakula na baadaye kuendelea na shughuli zao.
“Hivi ndivyo ninapenda kufanya, nilishawahi kumwambia hata Didier kuwa aniache nifanye kinachonivutia. Napenda kusaidia watu na moyo wangu unakuwa na raha katika hali hii,” alisema Clotilde ambaye ni mahiri jikoni.
Kikubwa kinachomsikitisha ni kuona mwanaye pamoja na kuwa mjini hapa, hataweza kula chakula cha asili anachokipika.
“Lakini Didier lazima ale chakula cha kambini kama wengine. Lakini wanapokula mashabiki ninakuwa nimemuunga mkono yeye pamoja na taifa langu,”alisema Clotilde.
0 Comments