HOFU YA WAPINZANI KUCHUKUA NCHI YAZIZIMA, WABUNGE WAKE WAPINGA MABADILIKO YA KATIBA NDANI YA CHAMA
Waandishi Wetu, Dodoma
MSUGUANO mpya umeibuka ndani ya (CCM) baada ya Kamati ya Wabunge wa CCM kupinga mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ya chama hicho yanayowaondoa kuwania nafasi za chama, huku wakihoji uongozi ulikopata mamlaka ya kufanya marekebisho hayo bila kuwashirikisha.

Suala la mabadiliko hayo ni miongoni mwa mambo yaliyotarajiwa kuibuka katika mkutano wa wabunge hao na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ambao ulitarajiwa kufanyika jana usiku kwenye ukumbi wa mikutano wa chama hicho uliopo makao makuu, Dodoma.

Mkutano huo wa Rais Kikwete na wabunge wa chama chake, unatangulia vikao vya juu vya chama hicho, ambavyo ni Kamati Kuu ya CCM (CC) inayotarajiwa kukutana leo na ukifuatiwa na Halmashauri Kuu (NEC) kesho, ili kubariki mabadiliko hayo ya Katiba ya CCM.

Habari kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika juzi usiku, zinasema wabunge hao walisema marekebisho hayo yamefanyika bila kuwashirikisha, hali inayowatia wasiwasi kwamba huenda CCM kikapoteza uongozi wa nchi.

Habari zaidi kutoka ndani ya kikao hicho zinasema, hofu kubwa waliyonayo wabunge ni mabadiliko makubwa yanayotarajiwa kufanywa katika katiba kwamba huenda yakabadili mfumo wa uchaguzi wa ngazi zote ndani wa CCM, huku wao wakiathirika kwa kiasi kikubwa.
Mchakato wa marekebisho hayo umekuwa ukifanywa na Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya CCM chini ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Pius Msekwa na matokeo ya kazi yake yatawasilishwa katika vikao vya CC leo na NEC kesho.


Miongoni mwa mabadiliko ambayo yamekuwa yakitajwa ni pamoja na wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuzuiwa kugombea nafasi yoyote ndani ya chama, ikiwa ni hatua ya kufanya mageuzi yenye lengo la kuondoa tatizo la baadhi ya watu kujilimbikizia madaraka.

Hata hivyo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana mjini Dodoma kwamba, mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa na NEC ya chama hicho ni kufanya wajumbe wa Halmashauri Kuu wachaguliwe katika ngazi za wilaya badala ya mkoa.



“Mimi nadhani hofu ya wabunge haina msingi, kwani hata kama wabunge watazuiwa ama hawatazuiwa kuwa viongozi wa chama katika ngazi hizo wanazozitaja si suala la kikatiba bali inaweza kuwa ni kanuni tu,” alisema Nape na kuongeza:

“Hata hivyo, watapingaje kitu ambacho bado hakijawasilishwa kwenye mkutano? Kama kuna mtu ana wazo hilo ataliwasilisha kwenye vikao, lakini nasema katiba haiwezi kumwengua mbunge katika kugombea nafasi yoyote ile, kinachoweza kumwengua ni kanuni.”

Nape alisisitiza kuwa, hadi jana hakukuwa na pendekezo lolote la kuwaengua wabunge katika kugombea nafasi za uongozi wa chama.

Hata hivyo alithibitisha kuwa uchaguzi ndani ya chama hicho unatarajiwa kufanyika kwa kuzingatia marekebisho yatakayofanywa, ambayo pia yanapendekeza wajumbe wa NEC kutoka katika jumuiya za CCM kuchaguliwa na jumuiya husika badala ya kupigiwa kura na Mkutano Mkuu.

Wabunge CCM
Inadaiwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Kapteni John Chiligati, alipata wakati mgumu kuwashawishi wabunge hao kukubali mabadiliko hayo bila mafanikio.
“Mimi kidogo nimwambie wewe (Chiligati) ulikuwa miongoni mwa waliokuwa kwenye mikakati ya kumwangusha JK (Jakaya Kikwete). Haiwezekani wakajifungia ndani na kufanya mabadiliko wanavyotaka,” alidokeza mbunge mmoja.

Taarifa hizo ziliwanukuu wabunge hao wakidai kuwa suala hilo linahitaji mjadala wa kitaifa ili kutoa wigo mpana kwa wanachama kutoa mawazo yao.

“Mnafanyaje mabadiliko bila kutushirikisha, unashika dola kwa kuwa na wenyeviti wa matawi ya CCM? Lazima uwe na wabunge ndiyo ushike dola, sasa mnatupuuza halafu mnakwenda kutuengua pembeni bila kutushirikisha, hatuwezi kukubali,” chanzo chetu kilimnukuu mmoja wa wabunge akilalamika na kuongeza:

“Kama mnasema nafasi za chini zitenganishwe, basi iwe hivyo kwa ngazi za juu kwa mwenyekiti na Rais na yenyewe itenganishwe muone moto utakaowaka.”

Hata hivyo, wabunge hao wamekubali mfumo wa kupata wajumbe wa NEC kutoka wilayani kuendelea, lakini wakakataa jinsi ya kupata wajumbe wengine na kutaka mjadala wa wazi kwa wanachama wao.
Kwa mfumo ulivyo sasa, mbali na wabunge kuruhusiwa kuchaguliwa kuwa wajumbe wa NEC, pia wana wawakilishi 20 kupitia kamati yao ambao huingia katika chombo hicho cha kufanya uamuzi ndani ya CCM.

Viti maalumu
Katika hatua nyingine wabunge wa Viti Maalumu CCM nao walitaka yafanyike mabadiliko kwenye kanuni ambayo nayo inatarajia kuwekwa ndani ya katiba ya chama hicho ya kuwataka kuwa na ukomo wa nafasi zao.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambayo yatapitiwa na CC leo, pamoja na kupitishwa na NEC kesho ni kwamba mwisho wa wabunge wa Viti Maalumu utakuwa ni miaka 10.

Kwenye Kamati ya Wabunge wa CCM, wa UWT, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ya Wanawake, Sophia Simba aliwashawishi wabunge waongeze kipindi hicho, lakini hoja yake iligonga mwamba.

Simba aliingiza tena ajenda hiyo katika kikao cha wabunge wote wa CCM kilichokutana juzi jioni chini ya Chiligati, lakini wazo hilo pia lilipata upinzani mkali kutoka kwa wabunge.

Kutokana na hali hiyo, Simba, Anna Abdalah, Diana Chilolo na wabunge wengine waliotumikia nafasi zao kwa vipindi viwili, huenda ubunge wao ukafikia ukomo baada ya kipindi cha sasa, hivyo wakitaka kuendelea lazima warejee kugombea nafasi hizo majimboni au kusubiri huruma ya rais katika nafasi zake za uteuzi.

Habari kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM, zinasema walioongoza kupinga kuongezwa kwa muda huo ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na yule wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela ambao waliungwa mkono kwa asilimia kubwa na wabunge vijana.

“Kwa ujumla kila mahali jamaa alikuwa anagonga mwamba na tumejipanga vikali kumweleza mwenyekiti kupitia wabunge wanaoingia ndani Halmashauri Kuu na Kamati Kuu kuwa lazima mambo haya yaondolewe,’’ alisema mmoja wa wabunge.

Mbunge huyo alisema mambo mengi ambayo yalikuwa yamependekezwa na kupelekwa kwa wabunge wa chama hicho yalionekana hayana maana kwani yalikuwa yakiwanyima haki.Alisema kuwa wabunge walisimama na kumweleza Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa hawana mpango wa kuendelea kujadili mambo ya katiba ya CCM na badala yake wakamtaka aishauri Serikali ili iendelee kushughulikia kero za wananchi.

Hata hivyo, hata kabla ya kuanza kwa vikao hivyo, Rais Kikwete alikutana na wabunge hao jana usiku, kikao ambacho kilielezwa kuwa ni cha kuweka mambo sawa kabla ya kuanza kwa vikao vya juu vya chama hicho.