MUFTI Mkuu wa Tanzania, Shehe Issa Shaaban Simba, amewataka Waislamu kote nchini kudumisha ushirikiano na dini zingine na makundi mangine ya kijamii na kuwa mstari wa mbele katika kujenga umoja.

Alisema hayo juzi katika nasaha zake katika Viwanja wa Msikiti wa Manyema, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wakati wa mkesha wa sherehe ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) iliyofanyika kitaifa wilayani humo.

Pia aliwataka Waislamu kutoa kipaumbele katika elimu hasa kwa kuwasomesha zaidi watoto wa kike sawa na wa kiume bila ya kuwabagua kama ilivyokuwa ikifanyika kabla ya kuja kwa Mtume Muhammad (SAW) ambaye alipinga jambo hilo na kuweka usawa baina yao.

Mufti pia aliwataka waumini hao kutowabagua wanawake na watoto wa kike kwa masuala ya mirathi kwa kuwa kuendelea na vitendo hivyo ni ubaguzi, ambao ulipingwa na Mtume aliyesisitiza umuhimu wa kuwaunganisha Waislamu wote. 
Sherehe hizo zilihudhuriwa na waumini mbalimbali kutoka mikoa kadhaa za Tanzania Bara akiwemo Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera pamoja na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo ambaye pia ni Mbunge wa Kilosa. “Watu wapendane, waungane wawe kitu kimoja, hiyo ndiyo njia ya ambayo Mtume aliifuata wakati huo.



Hakuna Uislamu wa mtu mmoja mmoja…haufiki mbali, lazima uwe na wenzio, lazima ushikamane na wenzako katika kuwa na umoja,“ alisisitiza Mufti. Alisema faida moja ya kushikamana ni Waislamu kuwa na sauti moja itakayosaidia wasikike katika mambo wanayohitaji kufanyiwa kwa kuwa wengi wana elimu ya kutosha.

Akisisitiza suala la umoja, alisema Waislamu hawawezi kukwepa kuungana hasa kwa kuzingatia kuwa mataifa mengi yakiwemo ya Ulaya yanaungana kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuwa na nguvu katika masuala mbalimbali.

Alisema Mtume Muhammad (SAW) ndiye aliyeleta mafundisho ya kuwaunganisha na suala hilo hivi sasa linafanyika pia katika nchi za Ulaya. “Kwa pamoja sasa tuibebe ajenda hii, badala ya kugombana tuenzi matendo ya Mtume ya kuendeleza umoja na makundi mengine, ili kupata heri ya mbinguni,” alisema Mufti.

Pia alikemea masuala ya ushirikina kwa Waislamu akisema Mtume Muhammad (SAW) alihimiza kumwamini Mungu pekee. Awali Mjumbe wa Baraza la Maulamaa, Shehe Hamid Jongo alitaka Waislamu kuondokana na chuki na madhehebu mengine kwa vile mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW) yalitawaliwa na kuwapenda watu wote bila kubagua dini zao wakiwemo Wakristo. 
Wakristo hawana chuki na Waislamu, bali watu wenye chuki na Uislamu ni Wayahudi…lakini Wakristo wapo karibu sana na wana mapenzi na Uislamu,” alisema Shehe Jongo. Shehe Jongo aliwapongeza watu wote walioshiriki kuchangia kwa hali na mali kufanikisha sherehe hiyo wakiwemo Wakristo, kitendo alichosema kimeonesha umoja baina yao na Waislamu.

Katika sherehe hizo, vikundi mbalimbali vya madrasa na wanazuoni walicheza Kaswida huku wengine wakionesha umahiri katika kuhifadhi Korani Tukufu mbele ya Mufti na viongozi wengine pamoja na mamia ya waumini waliojitokeza kusherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW).

Juzi Mufti wa Tanzania kabla ya kuwasili mjini Kilosa, alifungua Msikiti wa Dumila, Mvumi na jana aliweka jiwe la msingi la kuanza ujenzi wa Ofisi ya Bakwata ya Wilaya ya Kilosa na pia kuzindua rasmi Msikiti wa Manyema wa Wilaya ya Kilosa.

Boko Haramu walaaniwa KUTOKA mkoani Arusha, Mwandishi Wetu, John Mhala anaripoti kuwa viongozi wa dini ya Kiislamu waliongoza kongamamo maalumu la kulaani mauaji yanayofanywa na kikundi kidogo cha Kiislamu chenye msimamo mkali cha Boko Haramu nchini Nigeria dhidi ya madhebebu ya dini ya Kikristo.

Wakizungumza katika kongamano la amani lililofanyika katika Msikiti Ah Madiyya jijini Arusha, viongozi hao walisema hakuna maagizo ya Mwenyezi Mungu yanayotoa mamlaka kwa kikundi hicho ama mtu yeyote kutekeleza mauaji hayo dhidi ya waumini wa dini nyingine. Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa madhehebu ya Ahmadiyya nchini, Tahir Mohmood Choudhly aliwaomba Waislamu kote duniani kuungana na kulaani vitendo vya kinyama kama hivyo vinavyofanyika kwa kutumia mgongo wa Uislamu. 

Aliwaomba Watanzania kuwalilia wananchi wote waliouawa na kikundi hicho na kuiomba Serikali ya Nigeria kudhibiti mauaji hayo na kukishughulikia kikundi hicho kinachotumia mgongo wa Uislamu. “Sisi Waislamu tufike mahali tuelezane ukweli kwani matukio mengi ya uvunjifu wa amani yakiwemo kujilipua yanasababishwa sana na waumini wenzetu, hakuna maandiko yanayoagiza dini ya Kiislamu iteketeze dini nyingine, ‘’ alisema Choudhly.

Aliwataka viongozi wa madhehebu ya dini nchini kusimama imara kutetea amani na kujiepusha na uchochezi, kwani Taifa linawategemea sana katika kuepusha machafuko yanayoweza kuibuka. Pia aliwataka wananchi kuheshimu viongozi waliopo madarakani na kuacha kupinga kila kitu kinachotamkwa na kiongozi aliyeko madarakani, badala yake watoe mchango wa kusukuma maendeleo ya Taifa hadi utakapofanyika uchaguzi mwingine.

Naye Shehe Mkuu wa Kanda ya Kaskazini, Mzafara Ahamad alisema kuwa lengo la kongamano hilo lililowashirikisha viongozi mbalimbali wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kiislamu nchini ni kutoa mada ya kuomba amani na kulaami mauaji ya kikatili yanayoongozwa na kikundi hicho nchini Nigeria. Alisema kongamano hilo limefanyika pamoja na uzinduzi wa Msikiti huo wa Ahmadiyya Muslim Jamaint uliokarabatiwa kwa Sh milioni 70.