WAKATI Taifa likikabiliwa na wimbi la ubadhirifu wa mali ya umma hasa katika serikali za mitaa, walinzi wa sungusungu mkoani hapa, wanatuhumiwa kumkamata mtuhumiwa wa wizi wa kuku, Mipawa Samwel na kumhoji; alipokiri wakampiga na kumwua.

Akizungumza jana kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ofisa Mnadhimu wa Polisi wa Mkoa, Yusufu Mruma alisema Samwel alikamatwa na sungusungu mwishoni mwa wiki iliyopita na kuhojiwa kwa kuhusika na wizi wa kuku bila kumtaja aliyeibiwa.

Kwa mujibu wa Mruma, baada ya mahojiano kati ya sungusungu hao na Samwel ambaye ni mkazi wa Utura, mtuhumiwa alikiri kutenda wizi huo.

Tofauti na ilivyotarajiwa kwa mtuhumiwa kufikishwa katika vyombo vya sheria ili achukuliwe hatua, Mruma alidai kuwa sungusungu hao walimpiga mtuhumiwa na kumwua. Baada ya mauaji hayo ambayo ni kinyume cha sheria, Mruma alidai sungusungu hao walikimbia kusikojulikana na sasa Polisi inawatafuta ili wawafikishwe katika vyombo vya sheria kwa tuhuma za mauaji.  
Mbali na mauaji hayo, Mruma alisema Mihangwa Gitti, mkazi wa Uyui naye aliuawa bada ya kutuhumiwa uchawi.

Mruma alisema Mihangwa ambaye ni mwanamke, alivamiwa nyumbani kwake Jumapili iliyopita na kuuawa kwa mapanga.

Alisema baada ya kufanya mauaji hayo, wauaji walikimbia kusikojulikana na Polisi inaendesha na msako dhidi yao. Serikali mara kwa mara imekuwa ikikemea vitendo vya raia hata askari kujichukulia sheria mkononi, kwa kuadhibu watuhumiwa na badala yake kuwataka wawafikishe katika vyombo husika ili sheria ifuate mkondo.

Vibaka na wezi wamekuwa wakikamatwa katika baadhi ya maeneo nchini na kuuawa kisha kuchomwa moto kwa visingizo mbalimbali kutoka kwa raia wanaojiita wenye hasira kali, vikiwamo vya Polisi kuwakamata na kuwaachia
.