Nderitu Njoka, mwenyekiti wa chama cha wanaume akimfariji baba aliyepigwa na mkewe.
Waume nchini Kenya wanapanga kugomea vyakula vya mabibi zao kwa siku sita kutoka na kuongezeka kwa visa vya wanawake kuwapiga mabwana zao.
Badala yake wanaume watakuwa wakila mahotelini na magengeni
Mwenyekiti wa Chama cha maendeleo ya Kina baba Nderitu Njoka amesema mgomo huo wa siku sita una lengo la kuwashinikiza wanawake kukoma kuwanyanyasa na kuwapiga waume zao.
Kiongozi huyo Nderitu Njoka amesema kuanzia leo jumatatu ataanza kampeni ya kuwashawishi akinababa kula mahotelini badala ya majumbani mwao.
Mwenyekiti huyo wa maendeleo ya wauaume alikuwa akizungumza katika hospitali kuu ya mjini Nakuru huko Rift valley ambako alikuwa amekwenda kumliwaza baba mmoja ambaye amelezwa humo kutokana na kipigo alichopewa na mkewe.
Baba huyo akizungumza kwa uchungu hospitalini alisema mkewe alimuita nyumbani it akachukuwe pesa kabla ya kumfungia chumbani na kumtandika.
Kwa muujibu wa bwana Nderitu Njoka, mkoa wa kati nchini Kenya ndio unaongoza kwa idadi ya akina baba wanaopigwa na bibi zao.
Katika mkoa huo wa kati wanaume karibu nusu milioni wameripoti kutandikwa.
Chama hicho cha wanaume kimedai kuwa kuna wanaume ambao wanalazimishwa kufuo nguo za wake zao.
Wengine pia wamedai kunyimwa tendo la ngono na mabibi zao.
Jijini Nairobi wanaume ambao huona kivumbi kutoka kwa wake zao ni laki tatu.
Lakini baadhi ya akina mama kutoka mkoa huo wanasema akina baba ndio wa kulaumiwa kwa kushindwa na majukumu yao ya kifamila.
Wanasema waume wangi wamekuwa waume suruali tu.
Hata hivyo wengi wanasubiri kuona kama kweli mgomo huo utafaulu, na ni wanaume wangapi walio na pesa za kwenda kula hotelini badala ya kula majumbani mwao.
0 Comments