Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake itahakikisha kuwa mikataba ya uzalishaji gesi asilia iliyogunduliwa na makampuni binafsi nchini inawanufaisha ipasavyo wananchi wa Tanzania.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ambako gesi asilia imegunduliwa ama inatafutwa katika Bahari ya Hindi dhidi ya tishio ya uharamia wa Kisomalia.

Rais Kikwete amesema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Kampuni ya British Gas International (BGI) ukiongozwa na Sir Robert Wilson ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya British Gas (BG) Group ya Uingereza ambayo ni kampuni mama ya BGI.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jioni ya jana, Jumatatu, Februari 20, 2012, Ikulu, mjini Dar es Salaam, Rais Kikwete aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali yake itahakikisha kuwa Mikataba ya Pamoja ya Uzalishaji – Production Sharing Agreement (PSA) ambayo Tanzania itaingia na makampuni binafsi yanayotafuta ama kugundua gesi asilia nchini italenga kunufaisha pande zote mbili, yaani wananchi wa Tanzania na wawekezaji.

“Ninataka kuwahakikishieni kuwa tutahakikisha kuwa mikataba tutakayoingia ya uzalishaji wa pamoja – PSA- itawanufaisha wananchi wa Tanzania na vile vile wawekezaji kwa namna ambayo kila upande utajiona unanufaika, “ amesema Mheshimiwa Rais Kikwete katika mazungumzo hayo yaliyochukua zaidi ya saa moja.

Katika mazungumzo hayo, Sir Robert Wilson alimthibitishia Mheshimiwa Rais kuwa kampuni yake imefanikiwa kugundua kiasi kikubwa cha gesi asilimia katika visima vitatu vilivyochimbwa mwaka juzi na mwaka jana katika Bahari ya Hindi, kikiwamo kisima cha kwanza kabisa katika Tanzania kuchimbwa kwenye kina kirefu zaidi cha maji (deepwater well).

Sir Robert Wilson alimwambia Rais Kikwete kuwa kampuni yake iliwekeza dola za Marekani milioni 500 katika utafutaji gesi nchini Tanzania mwaka jana na kuwa itawekeza kiasi hicho hicho kwa mwaka huu.

Hata hivyo, Sir Robert Wilson ambaye alifuatana na ujumbe wa watu saba akiwamo Balozi wa Uingereza katika Tanzania, Bibi Diane Corner alimwambia Rais Kikwete kuwa katika nusu ya pili ya muongo wa sasa, BGI itaanza kuwekeza kiasi kikubwa zaidi, kiasi cha kati ya dola za Marekani bilioni 10 hadi 20, katika shughuli hiyo na katika uchumi wa Tanzania.

Sir Robert Wilson amesema kuwa kiasi hicho kitakuwa kikubwa mno kiasi cha kwamba Serikali ya Tanzania inatakiwa kuanza kujiandaa sasa kwa ajili ya uchumi wake kupokea kiwango kikubwa kiasi hicho cha fedha kwa wakati mmoja.

Sir Robert Wilson pia aliitaka Serikali ya Tanzania na BGI kuchukua hatua za kukabiliana kwa pamoja na changamoto ambazo zinakabili utafiti, utafutaji na hatimaye uzalishaji wa gesi asilimia katika Bahari ya Hindi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na tishio la uharamia wa Kisomalia, kulazimika kwa makampuni binafsi kutumia walinzi wao kujihami dhidi ya uharamia huo, kiasi kikubwa cha uwekezaji kitakachoingizwa katika uchumi wa Tanzania katika miaka michache ijayo kupitia gesi asilimia na uwezekano wa kutokea mivutano ya kimikataba kama ilivyotokea kwa makampuni ya madini.

Rais Kikwete amemhakikishia Sir Robert Wilson kuwa Serikali yake itachukua hatua stahiki kukabiliana na changamoto hizo. Mazungumzo hayo ya Rais Kikwete na ujumbe huo wa BGI yalihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mustafa Mkullo na Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa William Njeleja.

BGI iliingia katika Tanzania mwaka jana kwa kununua asilimia 60 ya hisa za kampuni ya Ophir Tanzania Limited ambayo tokea miaka ya 2005 na 2006 iliingia katika mikataba ya PSA na Serikali ya Tanzania na Shirika la Mendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa ajili ya ufatutafuji gesi katika vitalu vitatu katika Bahari ya Hindi.

BG Group ni moja ya makampuni makubwa zaidi katika biashara ya nishati duniani ikiwa na shughuli katika zaidi ya nchi 25 duniani. Ni miongoni mwa makampuni 15 makubwa zaidi katika Uingereza ikiwa na mtaji wa kibiashara unaokadiriwa kuzidi dola za Marekani bilioni 70.

Ingawa Tanzania imepata kugundua gesi katika maeneo ya Songosongo na Mnazi Bay lakini visima hivyo ni visima vya Serikali na BGI inakuwa kampuni binafsi ya kwanza kutafuta na kugundua gesi katika Tanzania.

                                                                          Mwisho.

Imetolewa na:Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,Ikulu.Dar es Salaam.21 Februari, 2012