Rais Jakaya Kikwete akizindua ya Benki mpya ya First National Bank (FNB), jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa First Rand Group ya Afrika Kusini, ambayo ni kampuni mama ya FNB nchini,Sizwe Nxasana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ,Elizabeth Nyambibo. Picha na Said Powa.

Festo PoleaRAIS Jakaya Kikwete amekiri Serikali yake kushindwa kufanya vizuri katika sekta ya umeme na reli na kuiangukia First National (FNB), kuwekeza katika sekta hizo.Kikwete alitoa kauli hiyo ya kukiri katika sekta hizo wakati wa uzinduzi wa benki ya FNB ya Afrika Kusini, jijini Dar es Salaam jana.

“Ni kweli kwenye reli na umeme tumefeli hivyo kama FNB mtaweza kuwekeza kwa ushirikiano na Tanzania katika sekta hizo mnakaribishwa; Kama mtaona mnaweza kuwekeza kwa pamoja katika miundombinu na sehemu za bandari nasema asante na mnakaribishwa,’’ alisema Rais Kikwete.

Kiwete alikumbusha kuwa katika salamu zake za mwaka mpya alisema kwamba serikali inaangaliuwa uwezekano kupunguza gharama za kufanya biashara nchini kwa kuwa inatambua kuwa hakuna maendeleo bila uwekezaji.

“Sekta ya kibenki ni sekta muhimu kwa kuwa ndiyo sekta inayoandaa mipango kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini, hadi sasa kuna benki binafsi 47 zinazofanya kazi nchini na katika hilo ninafuraha kwa kuwa sekta za kibenki zinafanya vizuri na biashara zinakwenda vizuri,” alisema Rais.



Alifafanua kuwa jambo hilo litakuwa sura nzuri katika kujitangaza na kuvutia wawekezaji zaidi kupitia wawakilishi wa benki ya FNB.Katika uzinduzi huo Rais Kikwete alizitaka pia benki nchini kutoa huduma za mikopo kwa sekta za uzalishaji, kilimo na viwanda ili kusaidia sekta hizo kukuza uchumi..

Alisema kuwa asilimia 70 ya Watanzania wanategemaa kilimo kwa kuwa ndiyo uti wa mgongo katika uchumi, hivyo huduma za mikopo zikitolewa kwa wakulima zitawawezesha kununua vifaa na mahitaji muhimu yatakayosaidia kunyanyua uzalishaji, kuboresha kilimo na uchumi kwa ujumla.

Kikwete pia alikubali benki hiyo kuwekeza katika miradi ya miundombinu na maeneo ya bandari ikiwa itaweza kuwekeza kwa pamoja.Naye Balozi wa Afrika Kusini nchini, Henry Chiliza alisema kuanzishwa kwa benki hiyo nchini kutasaidia katika ukuaji wa uchuni na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo na Serikali zake.

“Kwa Afrika Kusini benki hii imeshatoa ajira kwa watu wengi hivyo kuwekeza Tanzania, Watanzania wengi wataajiriwa jambo ambalo litasaidia katika sekta ya ajira.

Mkurugenzi wa benki hiyo, Size Nxasana alisema benki hiyo inatarajia kujitanua zaidia katika miji mbalimbali nchini na ikitarajia kuwekeza katika miradi ya umeme, reli, bandari na miundombinu.