SERIKALI imetangaza kuondoa zuio lililokuwa limewekwa kwa muda la kusitisha usafirishaji na uuzaji wa mahindi nje ya nchi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya serikali kufanya tathmini na kubaini kwamba wakulima wanahitaji fedha kwa ajili ya kununua pembejeo kwa ajili ya msimu wa Kilimo 2011/2012. Lakini pia hatari ya kuwapo njaa katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Shinyanga na Mara imeondoka kutokana na mvua nzuri za vuli zinazoendelea kunyesha.
Akiahirisha Mkutano wa Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema pia kwamba mahindi mengi bado yapo mikononi mwa wakulima katika mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Iringa na Mbeya kiasi kwamba hata Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) hautaweza kuwafikia wakulima wote katika muda muafaka na kununua
mahindi yao.
Aliwahimiza wakulima na wafanyabiashara kwa pamoja kutumia fursa hiyo kuuza mahindi, kununua na kusafirisha popote nchini na nje ya nchi kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizopo. “Ni matumaini yangu kuwa wafanyabiashara wote wenye nia ya kufanya biashara ya mahindi ndani na nje ya nchi watazingatia maelekezo ya Serikali kuwa bei ya kununulia mahindi isiwe chini ya Sh 350 kwa kilo na kuwalipa wakulima fedha taslimu badala ya kuwakopa,” alisisitiza.
Alisema Serikali inatambua kuwa kuondolewa kwa zuio hili kutaleta changamoto nyingi hasa katika maeneo ya mipakani na yenye uhaba mkubwa wa chakula. Aidha, aliwataka viongozi katika ngazi zote wahakikishe utaratibu mzima wa kununua mahindi unasimamiwa kwa umakini mkubwa ili kunufaisha wakulima wengi masikini vijijini.
“Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inaagizwa kutoa mwongozo mahsusi kuhusu utaratibu wa usafirishaji na uuzaji wa mahindi nje kuainisha wajibu na majukumu ya watendaji katika kila ngazi kuanzia vijiji, wilaya hadi mkoani ili kuepuka urasimu usio wa lazima kwa wakulima
na wafanyabiashara watakaoshiriki,” alisema Pinda.
Kuhusu tathmini ya hali ya chakula alisema inaonesha dalili nzuri za kuwapo chakula cha kutosha katika maeneo mengi nchini, lakini alisema ni vizuri kuendelea kutumia chakula kilichopo kwa uangalifu.
Akizungumzia pembejeo, aliwataka viongozi katika ngazi zote kuanzia watendaji wa vijiji, kamati zinazosimamia mpango wa pembejeo, uongozi wa wilaya, mikoa na wizara wahakikishe wakulima wanapata pembejeo kwa wakati. Katika suala la mifugo alisema zipo fursa nzuri ya kutumia rasilimali ya mifugo ambayo iko kwa kiasi kikubwa nchini na kutaka wananchi hususan wafugaji waelimishwe kuhusu kanuni za ufugaji bora wenye tija.
“Tuanzishe mashamba darasa ya mifugo katika Halmashauri na majimbo yetu kuonesha umuhimu wa kutumia mifugo tuliyonayo kwa tija zaidi na hivyo kujiletea maisha bora,” alisema. Alizungumzia pia fursa ya kuanzisha ufugaji samaki na viumbe wa majini kwa kuhamasisha wananchi kupenda shughuli za uvuvi kwa njia halali na ufugaji samaki ili kujipatia kipato na lishe bora.
“Aidha, tuendelee kuhamasisha wananchi juu ya faida na umuhimu wa kuanzisha ufugaji nyuki na kuendesha ushirika wa wafugaji nyuki. Tushirikishe wananchi kutumia kanuni bora za ufugaji wa zao hili. Halmashauri zitenge fedha na kuweka mikakati ya kukuza shughuli za ufugaji nyuki katika maeneo yao,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Akigusia mgomo wa madaktari, Waziri Mkuu alisema uligusa kila mtu na kushukuru kwamba sakata hilo sasa lina mwelekeo mzuri baada ya makubaliano ya msingi. “Ninachowaomba sasa wote twende tupeane moyo wa kufanya kazi na kuwasaidia wenzetu hususan wagonjwa ambao maisha yao yanategemea huduma ya madaktari,” alisema.
Yaliyojiri bungeni Katika Mkutano huo, maswali 119 ya msingi na 290 ya nyongeza yalipata majibu huku manane ya msingi na na nne ya nyongeza kupitia utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yalijibiwa. Miswada miwili ilisomwa kwa mara ya kwamba ambayo ni wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania wa Mwaka 2011 na wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wa Mwaka 2012 Miwili mingine ilisomwa na kujadiliwa katika hatua zote; Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Fedha Haramu wa Mwaka 2012 na wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2011.
Pia Azimio la Bunge kuhusu Mkataba wa Vijana wa Afrika wa Mwaka 2006 uliridhiwa sambamba na kujadili Azimio la Bunge la Kuridhia Marekebisho ya Jedwali la Nne la Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura ya 147. Azimio hili halikupitishwa kwa vile ilibainika kwamba halina maslahi kwa mwananchi wa kawaida.
Mgomo wa madaktari Katika mkutano huo pia wabunge walipokea Kauli ya Serikali kutoka kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii kuhusu mgomo wa madaktari. “Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tayari Serikali imechukua hatua mbalimbali za kumaliza
mgomo huu. Aidha, imeshughulikia baadhi ya madai ya madaktari na mengine yanaendelea
kushughulikiwa.
“Madaktari wetu wamerejea kazini leo na kuendelea kutoa huduma za tiba na hivyo kuokoa maisha ya wagonjwa wasio na hatia, ili wasiteseke na pia kuokoa maisha yao. “Serikali itaendelea kushirikiana na vyombo vyote kuhakikisha tatizo hili linapatiwa ufumbuzi wa kudumu,” alisema na kumshukuru Spika Anne Makinda, Kamati ya Bunge ya Huduma
za Jamii na wabunge kwa nia njema waliyoionesha katika kuhakikisha mgomo unafikia tamati.
“Nishukuru pia, makundi mbalimbali ya jamii wakiwamo viongozi wa dini, madaktari wa Jeshi, madaktari bingwa, wauguzi ambao pamoja na hali yote ilivyokuwa walionesha nia ya
kuwasaidia wananchi ambao walihitaji huduma wakati wa mgomo huu.
“Niwashukuru pia wananchi wote kwa uvumilivu wao. Ni dhahiri tumejifunza mengi, na wajibu wetu kama Serikali ni kuhakikisha kwamba hali kama hii haijirudii tena,” alisema. Waziri Mkuu aliahirisha Bunge hadi liahirishwe hadi Aprili 10 saa tatu asubuhi, litakapokutana mjini hapa.
0 Comments