Umoja wa mataifa umetangaza kuwa baa la njaa nchini lililotangazwa kukumba taifa la Somalia sasa limefikia kikomo.
Umoja huo umesema hali imeimarika nchini humo kutokana na mavuno mazuri na misaada ya kibinadamu inayoendelea kutolewa.Mwezi uliopita mshirikishi mkuu wa shughuli za umoja uhuo nchini Somalia Mark Bowden alisema maelfu ya watu wamekufa tangu mwezi julai mwaka uliopita kutokana na baa la njaa. 
Afisa mkuu wa shirika la umoja wa mataifa kuhusu chakula na kilimo FAO Jose Granziano amesema mvua kubwa iliyonyesha pamoja na misaada ya kibinadam iliyotolewa imechangia pakubwa kuimarika kwa hali ya maisha nchini somalia.
Amesema maisha ya watu wengi yameokolewa lakini akaonya kuwa ikiwa mvua inayotarajiwa kunyesha tena haitatosha, basi hali hiyo hiyo huenda ikarelejea tena katika kipindi cha majuma kadhaa.
Watu bado wanaendelea kufa kutokana na athari za ukame huo na vita. Zaidi ya watoto elfu mia moja wanakabiliwa na tishio la kuangamia kutokana na utapia mlo.
Amesema utafutaji wa suluhu ya mzozo wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya miongo miwili nchini Somalia utachanga pakubwa kuimarika kwa hali ya maisha nchini humo.