MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari, amesema sera mbaya za Serikali katika mishahara zimesababisha mgomo wa madaktari.
Amesema sera hizo zimesababisha mkanganyiko mkubwa katika mishahara na kuibua manung’uniko katika baadhi ya sekta na hatimaye migomo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika viwanja vya Keko Magorofani juzi, Profesa Safari alisema sera hizo zimesababisha kuwe na viwango tofauti vya mishahara kwa baadhi ya watumishi wa umma.
Alitoa mfano wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao alisema wanalipwa mishahara mikubwa tofauti na watumishi wengine wa sekta za umma.
“Mimi ni Profesa wa chuo kikuu lakini mshahara wangu haufiki hata Sh2 milioni lakini huko BoT na TRA kuna watu wa kada za chini kabisa wanalipwa mamilioni ya pesa,”alisema Profesa Safari.
Profesa Safari ambaye alikuwa akizungumza kwenye kampeni maalumu ya chama hicho ijukanayo kama ‘Ondoa CCM Dar’ alisema mgomo wa madaktari unaoendelea sasa ni matokeo ya sera mbovu za mishahara zilizowekwa na Serikali.
Katibu wa Chadema katika Kanda ya Dar es Salaam, Henry Kileo, alisema Serikali ndiyo inayopaswa kulaumiwa kuhusu mgomo wa madaktari na kwamba wananchi wasio na hatia ndiyo wanaoumia.
“Hao viongozi na familia zao wakiumwa wanakimbilia nje ya nchi lakini walalahoi hawana pa kwenda na ndiyo wanaoumia,”alisema Kileo.
Alisema mfumo mbaya wa utawala uliowekwa na CCM, umesababisha maisha yawe magumu na taifa kukosa mwelekeo.
“Tutapambana kudai haki zetu za msingi na tukishindwa kuwaondoa kwa kura tutatumia nguvu ya umma,”alisema Kileo.
Kuhusu kampeni hiyo, Kileo alisema ina lengo la kukiimarisha chama na kujiandaa kwa chaguzi mbalimbali..
0 Comments