Wakereketwa wa haki za binaadam nchini Ukraine wametoa wito kwa rais wa taifa hilo, Viktor Yanukovych, kutokomeza ubaguzi wa rangi baada ya gazeti moja katika mji wa Ternopil, kuchapisha mchoro ulioonyesha wanafunzi wa kiume wa asili ya Kiarabu na Kiafrika wakimpigania msichana mwenye asili ya Ukraine.Katika mchoro huo wanafunzi hao wamechorwa kwa mfano wa nyani.
Gazeti hilo lijulikanalo kama Nowa Ternopil Hazeta, limesema kuwa hivyo ndivyo lilivyoamua kuonyesha jinsi mapigano kati ya wanafunzi wenye asili wa Kiafrika na Kiarabu katika klabu moja ya usiku mjini humo wakati wakinywa pombe.
Kwenye ukurasa wa kwanza kulikuwa na kichwa cha habari kisemacho "damu ya Waafrika na Waarabu ilimwagika wakipigania malaya wetu."
Mchoro huo pia ulionyesha nyani wawili wakimpapasa mwanamke mmoja mzungu, huku ukipachikwa kwenye picha nyingine tofauti ya wanafunzi Waafrika wakinywa pombe.
Gazeti hilo limejitetea likisema kuwa lilitaka kuonyesha tu kuwa mwanamume yeyote mlevi anaonekana kama nyani; maelezo ambayo hayajawaridhisha wanafunzi wa kigeni nchini humo.
Mohammed Sisey, mkuu wa Baraza la Waafrika nchini Ukraine, aliviambia vyombo vya habari nchini humo kuwa ni aibu kwa gazeti kutoka taifa kama hilo kuonyesha wazi ubaguzi wao wa rangi.
Alitoa wito kwa serikali kutoa maelezo rasmi ya kueleza kwa nini gazeti hilo lilifanya dharau hiyo.
Waendesha mashtaka katika mji wa Ternopil wamesema kuwa wanaendelea na kuchunguzi ili kuona kama wanaweza kufungua mashtaka ya uhalifu dhidi ya gazeti hilo.
0 Comments