Keneth goliama
WAFANYABIASHARA wa Soko la Machinga Complex jijini Dar es Salaam, wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kuivunja bodi ya soko hilo kwa madai kuwa imeshindwa kusimamia soko hilo baadhi ya wajumbe wake wakiendekeza rushwa.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana wafanyabiashara hao walidai kuwa uongozi wa soko hilo umeshindwa kuwahamisha wafanyabiashara wa Soko la Ilala Mchikichini kutokana na baadhi yao kupewa fedha.

Walisema kuwa imefika wakati sasa kwa Rais Kikwekwe kuwaonea huruma kutokana na baadhi ya vigogo wa bodi hiyo kutumia soko la Ilala kujinufaisha wakiliacha bila kulivunja ili wenzao wahamie soko Machinga Complex kama wao.

“Umefika wakati kwa Serikali kuvunja Bodi ya Machinga Complex na kuteua bodi mpya itakayosaidia kufikia mwafaka. Haiwezekani bodi hiyo ishindwe kuwahamisha wafanyabiashara soko la Ilala kwa miaka miwili huku sisi tukiteseka Machinga Complex kwa kukosa wateja,” Steven Bukosi anayefanyabiashara katika soko hilo.




“Viongozi wakuu wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wanachukua pesa kwa wafanyabiashara wa soko la Ilala, ndio maana hata ukiongea mkuu wa mkoa ananyamaza kimya”alidai mfanyabiashara mwingine.

Walisema sababu kuu ya baadhi ya wamachinga kushindwa kuingia Machinga Complex ni vigogo wengi kuchukua vizimba ambapo sasa inokekana kama vimejaa watu.

“Wanavunja kufuli na kuchukua kila kitu halafu wanawapa watu ambao siyo wafanyabishara na hawafiki,” alisema Zuhura Wiliam kwa niaba ya wenzake.Alisema kuwa Jiji linaonekana kushindwa kuendesha soko hilo na kwamba ni bora wapewe na kuliendesha wao.


Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Machinga Complex, Abubakar Rakesh alisema viongozi wa juu wanajua mambo yote katika soko hili lakini wamekuwa waoga.

Alisema licha ya ushauri kutolewa kuhusu soko hilo lakini hakuna kiongozi yoyote anayethubutu kufanyia kazi.
Alisema dhamira ya Rais Kikwete kwa wamachinga inanyanganywa na wachache ambao hawataki kuona akina mama wanaohangaika wananufaika na biashara zao ndogo ndogo.

Alisema lengo la kutaka kupangisha ghorofa ya nne na tano ya soko hilo ni kuruhusu wafanyabishara wachache kuwekeza na kuuza vitu vya jumla ili kuvutia wateja.Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Sadik Meck Sadiki alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo hakupatikana baada ya simu yake kuita bila majibu.