Na Saleh Ally
TATIZO la kuanguka uwanjani kwa beki wa Bolton ya England, Fabrice Muamba na moyo wake kusimama, limefanya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kuweka msisitizo kuhusiana na afya za wachezaji.
Wiki iliyopita, Muamba alianguka ghafla na moyo wake kusimama wakati wa mechi ya Kombe la FA dhidi ya Tottenham Hostpur.
Msemaji wa Caf, Suleiman Habouba, ameliambia Championi Jumatano kuwa, ni lazima timu zote zinazoshiriki michuano chini ya shirikisho hilo kuhakikisha zinafanya vipimo sahihi vya wachezaji wao.
“Lazima wafanye vipimo na wanalijua hilo. Tumekuwa tukisisitiza lifanyike zoezi hilo lakini kuanzia mwaka huu tumekuwa wakali maana tumeona wachezaji wengi wanaanguka uwanjani.
“Pia tuligundua baadhi ya timu zilikuwa zinaleta vipimo ambavyo si sahihi, hivyo Simba, Yanga au timu yoyote itakayoshiriki michuano chini ya Caf lazima ifanye hivyo na safari ijayo huenda tukalisimamia zoezi hilo kwa ukaribu,” alisema Habouba.
Gazeti hili liliwatafuta madaktari wa timu hizo, Juma Sufiani wa Yanga na Cosmas Kapinga wa Simba ambao walikiri kulifanyia kazi agizo hilo la Caf.
“Kweli, Caf wamesisitiza na kuna fomu maalum ambazo wamekuwa wakitoa ambazo hutakiwa kuzijaza na kuziwasilisha TFF halafu zinatumwa kwao,” alisema Sufiani.“Kweli wamekuwa wakali sana na safari hii Caf wamesisitiza masuala mengi na ripoti yao imegawanyika katika makundi manne. Moja rekodi binafsi za mchezaji. Mbili, historia ya familia yake kama kuna magonjwa ya kifafa, moyo na mengine,” alisema Kapinga.
Aliongeza: “Tatu, kuangalia urefu, uzito, mifupa, misuli na vingine. Nne ni kuhusu mfumo, mfano mfumo wa damu, fahamu, chakula na mingine. Lengo ni kutaka kujua uhakika wa afya ya mchezaji.”
Simba inaendelea na michuano ya Kombe la Shirikisho na Jumapili hii itaivaa ES Setif ya Algeria wakati Yanga iling’olewa na Zamalek ya Misri kwa jumla ya mabao 2-1 katika michuano ya Ligi ya Mabingwa.
Kwa Tanzania, Nurdin Bakari akiwa Simba (sasa Yanga) na Kiggi Makasi wa Yanga, wamewahi kukumbwa na tatizo la ugonjwa wa moyo. Hata hivyo inaelezwa kuna wachezaji wengi wanacheza wakiwa na matatizo hayo bila ya wao kujua.
0 Comments