Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentekoste la Welfare Ministry of Africa, Stanley Mnai akivikwa pete ya ndoa na Bibi Harusi, Gloria Kaserwa katika kanisa hilo lililopo eneo la Vetenari, Temeke jijini Dar es Salaam wiki iliyopita. Katikati ni Askofu Msaidizi, Upendo Mnai, ambaye ni mama mzazi wa bwana harusi. (Na Mpigapicha Maalumu).


ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kipentekoste la Welfare Ministry of Africa, Stanley Mnai amefungishwa ndoa takatifu na mama yake mzazi ambaye pia ni Askofu Msaidizi wake, katika misa ya 40 Kibaha ndoa iliyofanyika makao makuu ya kanisa hilo lililopo eneo la Vetenari, Temeke jijini Dar es Salaam.

Kanisa hilo lililoanza rasmi mwaka 2009 na kuvuta waumini wengi, lina viongozi wawili tu wenye vibali rasmi vya kufungisha ndoa takatifu kanisani hapo, ambao ni Askofu Mkuu na Askofu Msaidizi.

Kwa sasa, Askofu Msaidizi ni mama mzazi wa Askofu Mnai aitwaye Upendo Mnai ambaye
alifungisha ndoa hiyo ya kwanza Jumapili iliyopita tangu awe askofu msaidizi, huku kukiwa na mahudhurio ya waumini wengi, wakiwamo ndugu, jamaa na marafiki wa maharusi.

Mvuto wa ndoa hiyo ya Askofu haukuwa kanisani tu, bali ulianzia wakati wa maandalizi, kwani tofauti na yalivyo mazoea ya kuona bibi harusi mtarajiwa akiandaliwa sherehe ya 'Kitchen Party’ na upande wake, hali ilikuwa tofauti kwa ndoa ya Askofu Mnai, kwani mama mkwe wa bibi harusi mtarajiwa, Gloria Kaserwa ndiye aliyeandaa shughuli hiyo kwa ajili ya binti anayetarajiwa kuolewa na mwanawe.

Aidha, licha ya kuwa Askofu, Mnai katika kipindi chote cha maandalizi ya ndoa yake, alikuwa akihudhuria mafunzo maalumu ya ndoa kutoka kwa mchungaji wake.

Siku ya harusi yake, Askofu Mnai aliyezaliwa miaka 30 iliyopita aliingia kanisani na
kupokelewa kwa hoi hoi, nderemo na vifijo majira ya saa 9.00 alasiri na ilipotimu saa 11, ndoa
ilifungishwa rasmi na Askofu Msaidizi yaani mama yake mzazi.

Mara baada ya tukio hilo, wanandoa na wageni waalikwa walihudhuria sherehe ya kukata na shoka iliyofanyika Ukumbi wa Hoteli ya Mwika iliyopo Sinza, jijini Dar es Salaam.

Wakati akiendesha ibada hiyo Mama Askofu Upendo, alisema: “Ndoa takatifu ina kibali mbele za Mungu, ndoa ni kitu endelevu, kila siku unajifunza kama shule inavyotaka, lakini leo tunashukuru tunahitimisha uchumba ili wapate baraka za kuwa mwili mmoja.”

Aliongeza kuwa, hesabu ya Mungu si kama ya wanadamu bali kwa Mungu moja na moja ni moja wala si mbili, kama kawaida ya hesabu tulizozizoea.

Alisema mwanaume ni kichwa cha nyumba, lakini hapaswi kuwa dikteta na kwamba kama akiwa hivyo, huyo hawezi kuwa kichwa cha nyumba tena, bali Simba, huku akionya kuwa,
'ubabe’ ndio unaosababisha ndoa nyingi kuwa na matatizo na hatimaye kuvunjika.
“Mungu amekutafutia mwanamke wa kufanana naye tabia na kuacha za awali kutoka kwa wazazi, sasa mwanaume kuwa ukiwa dikteta mkeo atakuwa hana likizo kwa mkubwa wake wewe, kumdharau ni kinyume cha mpango wa Mungu kwa kuwa huko si kufanana.”

Alisisitiza kwa maharusi hao kuwa kuolewa kuna raha sana kwa kuwa walioshibana kwa dhati na wanakuwa mithili ya watu wanaoishi peponi.

Mama Mnai alimsisitizia mkwe wake kumtii na kumpenda mume wake, akisema asipofanya
hivyo na kumtii, huenda akatoa mwanya kwa shetani kupata nafasi ya kuharibu ndoa na
kuzisambaratisha.

Huku akishangiliwa mara kwa mara, alionya kwa kusema; “Msiwachokoze waume zenu wasije wakajaribiwa na matokeo yake ni nyumba nyingi kuvunjika na kusababisha matatizo makubwa kwa jamii kama hili la watoto wanaoishi katika mazingira magumu, yaani chokoraa.”

Mmoja wa mashuhuda wa ndoa hiyo, Michael Sebastian (29) mkazi wa Temeke ambaye pia ni muumini kanisani hapo aliizungumzia ndoa hiyo kwa kusema: “Kwanza sijawahi kuona mafunzo ya maadili ya ndoa kwa mwanamke yakifundishwa na upande wa wakwe wa mwanamke.

“Na hata hili la mama kufungisha ndoa mwanawe wa kwanza kumzaa limenifurahisha na halitanitoka akilini mwangu, kwani kwangu ni moja ya maajabu ambayo nimezoea kuyaona kanisani hapa tangu nilipoamua kuokoka katika kanisa hili.”
Naye Mchungaji wa uchumba na ndoa, Peter Mwasandube alisema ilikuwa ni kitu cha
kumfurahisha sana na kuona anahitimisha harusi ya Askofu wake Mkuu kwani wakati wote
wa uchumba wao yeye ndiye alihusika kwa jambo lolote wakati wowote.

“Kwa hiyo sasa naona nitapumzika kidogo kwa kulifanikisha hili leo,” alisema. Kwa upande wa askofu Mnai na mkewe Gloria, waliahidi kuishi kwa maadili yanayopendeza duniani na mbinguni kwa msaada wa Mungu.

Alipoulizwa na mwandishi anajisikiaje baada ya kufungisha ndoa hiyo, Mama Mnai alisema,
“Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza, nimemaliza kazi ambayo ilikuwa ngumu kabla ya
kuifanya.”