JESHI la Polisi mkoani hapa linawashikilia watu wawili, mke na mume, kuhusiana na kifo cha mtoto mwenye umri wa miaka mitano ambaye ni bubu na mlemavu wa miguu aliyeuawa Machi 7 mwaka huu na mwili wake kutupwa katika choo cha shule ya Msingi Hombolo, nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Steven alisema jeshi lake linawashikilia Redience Charles (30) ambaye ni mama mzazi wa mtoto Karim Salum
aliyeuawa na Benjamin Chipanha (48) ambaye ni baba wa kambo wa mtoto huyo.
Alisema kuwa mwili wa marehemu huyo uligundulika Machi 21 mwaka huu, ukiwa kwenye
shimo la choo cha shule ya msingi Hombolo Bwawani “A”, lakini tayari ukiwa umeharibika vibaya baada ya kuwamo shimoni humo kwa takribani siku 14.Kamanda Zelothe alisema taarifa zaidi zinaeleza kuwa mama mzazi wa marehemu amekuwa akieleza kijijini hapo kuwa mtoto wake alikuwa amechukuliwa na wafadhili kwenda kulelewa mkoani Tanga, jambo ambalo Kamanda Steven alisema halikuwa la kweli.
Alisema kuwa uchunguzi wa kina wa tukio hilo la kusikitisha unaendelea na kwamba watuhumiwa hao wanalisaidia jeshi la Polisi na mara upelelezi utakapokamilika watuhumiwa
hao watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Aidha alimtaka mwananchi yeyote mwenye taarifa zaidi kuhusiana na tukio hilo kuwasiliana
na Polisi.
Taarifa za awali zilizomkariri diwani wa Hombolo Bwanani, Mussa Kawea zinadai mama wa mtoto, licha ya awali kudai mwanawe amepata mfadhili wa kumlea mkoani Tanga, alijua kwa
hakika mtoto huyo hakuwa kwa mfadhili yeyote.
Kawea anasema Machi 7 walipata taarifa za kupotea kwa mtoto huyo baada ya bibi yake mzaa
mama, Esther Kuyowona kutoa taarifa ya kutoweka kwa mjukuu wake na kwamba juhudi za kumdodosa mama wa mtoto zilipoonekana kutozaa matunda, walitoa taarifa Polisi.
Alisema pamoja na mama kudai mwanawe yupo Tanga, wananchi walifanya msako na
katika pitapita yao walisikia harufu kali katika choo cha shule na hivyo kutoa taarifa tena Polisi na hivyo kushirikiana kuvunja choo hicho na kukuta mabaki ya mwili wa mtoto huyo ulioharibika.
0 Comments