Na Musa Mateja
MASTAA wa Bongo, Wema Isaac Sepetu na Khalid Ramadhan ‘Tundaman’, wamekumbwa na skendo nzito wakidaiwa wapo katika uhusiano wa siri, Ijumaa Wikienda linakupasha.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Wema ambaye ni nyota wa sinema za Bongo na Tundaman msanii wa Bongo Fleva, walianza kufukuziana wakati Mbongo Fleva huyo alipokuwa nchini Uingereza kimuziki.
MWANZO WA SAFARI
Inadaiwa kuwa mastaa hao walianza kwa kuchati kupitia mtandao wa BBM unaopatikana kwenye simu za Blackberry na mara chache walipigiana simu na kukolezana kwa maneno matamu.
Chanzo kikadai kuwa, Tundaman aliporejea nchini Machi 15, mwaka huu, kabla ya kwenda kwake, Ubungo, Dar es Salaam, alimtafuta Wema ambaye alikuwa Mbezi Beach, Dar akirekodi sinema.
“Baada ya mawasiliano hayo kufungua ukurasa wa uhusiano, Tunda alirudi Bongo tarehe 15 Machi, moja kwa moja alimfuata Wema ambaye alikuwa Mbezi Beach, kule alimkabidhi zawadi alizotoka nazo UK (Uingereza),” kilisema chanzo kingine.
KUNA MTU WA KATI
Kwa mujibu wa madai yaliyopo mezani kwa gazeti hili, msanii wa filamu Bongo, Snura Mushi ndiye anayetajwa kuwaunganisha wawili hao. Snura na Tunda wana udugu wa kaka na dada.
“Snura ndiye amekuwa akimshawishi Wema kuwa na Tunda kwa sababu muda mwingi wako pamoja wakirekodi filamu za mnyange huyo wa Tanzania mwaka 2006,” kiliongeza chanzo chetu.
MADAI YAFIKA MEZANI KWA IJUMAA WIKIENDA
Machi 17, mwaka huu, Ijumaa Wikienda lilipata taarifa kutoka kwa chanzo kingine kikidai kuwa asubuhi ya siku hiyo (Jumamosi), Wema aliamkia nyumbani kwa Tunda, Ubungo.
Bila kupoteza muda, paparazi wetu alimvutia waya mlimbwende huyo na kumuuliza kuhusu madai hayo ambapo alikuja juu na kutaka kumjua mtoa habari hizo.
“Si kweli, nakataa. Halafu nani kawaletea hizo habari?” alihoji Wema.
Hata hivyo, kutokana na maadili ya kazi, Wema hakutajiwa mnyetishaji huyo.
Wakati gazeti hili likiwa katika uchunguzi wake kuhusu madai hayo, zikatua taarifa nyingine kuwa, Tunda amehamishia makazi yake nyumbani kwa Wema na kuwafanya mastaa hao kuishi kwa kupika na kupakua.
TUNDA MAN ATUA GLOBAL
Machi 24, mwaka huu, mhariri wa Ijumaa Wikienda alimwita msanii huyo kwenye ofisi za Global Publishers zilizopo Bamaga-Mwenge, Dar kwa lengo la kumsikia alichonacho kuhusiana na madai hayo.
Akizungumza kwa utulivu, Tunda alikataa kutoka kimapenzi na Wema ambaye mara ya mwisho alikuwa mchumba wa msanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond’.
UKARIBU WAKE NA WEMA
Tunda alisema alipokuwa nchini Uingereza alikuwa akiwasiliana sana na msanii wa sinema, Snura ambaye alisema wanaitana dada, kaka.
“Nilipokuwa Uingereza nilichati sana na Snura ambaye ni dada yangu, ikawa kila nikiona picha yake anakuwa pamoja na Wema, nikamuuliza (Snura), akasema yuko naye karibu kwa vile anashuti filamu yake.
“Nilipokaribia kurudi Bongo, dada Snura aliomba nimletee zawadi, nilimkubalia.
“Kwa hiyo siku niliporudi, sikutaka kwenda nyumbani (Ubungo) na zawadi zake kwa sababu kuna madogo kibao wangezichangamkia, nikamtafuta Snura kwa simu, akaniambia yupo Mbezi, nilikwenda kule na kumkuta na Wema.
“Nilimpa zawadi dada Snura, kisha nikaenda nyumbani.
Tunda aliendelea kudai kuwa, siku nyingine alikutana na Wema alipokwenda Mwananyamala Komakoma kwa Snura kwa ajili ya kula wali na maharage kwa kuwa anakipenda chakula hicho.
Alisema: “Ni kweli nimekuwa nikichati na Wema kwenye BBM, hata sasa hivi hapa nina meseji zake kwenye simu yangu.
Ijumaa Wikienda: Nani huwa anaanza kuchati na mwenzake?
Tunda: Mh! Inategemeana.
MASWALI MAGUMU
Hata hivyo, pamoja na utetezi wa Tunda bado kukawa na maswali magumu ndani ya utetezi wake.
Ijumaa Wikienda: Ulisema ulimpelekea zawadi Snura kabla ya kufika nyumbani kwako kwa vile una wadogo zako kibao wangezichangamkia?
Tunda: Ndiyo.
Ijumaa Wikienda: Unaishi na nani?
Tunda: Mtoto wangu wa mwaka mmoja na miezi kama mitatu na rafiki yangu Maneke (wa AM Records), lakini upande mwingine anaishi mchumba wangu.
Ijumaa Wikienda: Sasa mbona unaishi na watu wachache sana, hakukuwa na sababu yoyote ya kupeleka zawadi kwanza Mbezi kwa Snura, kisha urudi kwako.
Tunda: Aah! Niliamua kumpelekea kwanza, tena nilikwenda na Maneke.
Ijumaa Wikienda: Umesema huna uhusiano na Wema, kwa nini mnachati kwenye BBM, maana kumbukumbu zinaonesha uhusiano wake na Diamond ulianza kwa kuchati naye kama hivi?
Tunda: Si unajua tena.
0 Comments