Na Makongoro Oging’ LILE sakata la msichana Morine Amatus (22), anayetajwa kuwa ni mtoto wa Amatus Liyumba, aliyekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Lindi, akiwa na wenzake watatu, wakidaiwa kukutwa na madawa ya kulevya ya kilo 210 , yenye thamani ya shilingi Bilioni 9.4 limeingia katika sura mpya baada ya baba yake (Morine) kutakiwa kukamatwa, hivyo kuingia kitanzini.
Habari za uchunguzi kutoka ndani ya jeshi la polisi zinadai kuwa Liyumba anaingia kitanzini kwa kuwa anatakiwa akamatwe na ahojiwe kuhusiana na madawa hayo kwa kuwa mtoto wake amedaiwa kuhusika na tayari katupwa gerezani akisubiri kesi yake kusikilizwa.
Chanzo chetu ndani ya jeshi la polisi kimesema kumekuwa na shinikizo kutoka serikalini kwa waziri mmoja (jina limehifadhiwa) kutaka Liyumba akamatwe na kutupwa rumande kwa kile kilichodaiwa kuwa, ili upelelezi uweze kufanyika kwa kina.
Alipoulizwa kwa njia ya simu na gazeti hili Jumapili iliyopita, Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi, Godfrey Nzowa hakukiri wala kukataa kuhusu kukamatwa Liyumba ili uchunguzi ufanyike.
“Ninachoweza kusema ni kwamba uchunguzi juu ya tukio lile unaendelea. Kuhusu Liyumba ni kwamba mtoto wake ana miaka 22, hivyo ni mtu mzima kuna mambo anaweza kuyafanya bila baba yake kujua, lakini kama uchunguzi utatutaka baba yake akamatwe kuhojiwa, hatuwezi kushindwa kufanya hivyo,” alisema Kamanda Nzowa.


Alipododoswa zaidi, kamanda huyo alisema kwa kawaida polisi wanapofanya uchunguzi wao hawawezi kusema ni nani akamatwe na kuhojiwa na wala huwa hawasemi nani amewapa taarifa za mtu anayechunguzwa.
“Hizo ni kanuni zetu, hatuwezi kusema nani atakamatwa kwa jambo fulani au kumtaja mtu ambaye ametuletea taarifa za watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya na ndiyo maana tunafanya kazi vizuri sana, nawaomba wananchi wema wazidi kutupa ushirikiano,” alisema Nzowa.
Hata hivyo, Nzowa alifafanua kuwa kutokana na wingi wa madawa waliyokamatwa nayo, mtoto huyo wa Liyumba na wenzake, kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa itapelekwa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Watuhumiwa wengine waliokamatwa pamoja na Morine katika Kijiji cha Mchinga Mbili, Lindi kwa mujibu wa Nzowa na kufikishwa mahakamani ni Pendo Mohamed Cheusi (67), mkazi na mkulima wa kijiji hicho na Hemedi Said (27), dereva na mkazi wa Mtoni, jijini Dar es Salaam ambaye pia ni mtoto wa mwenye nyumba hiyo.
Aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Ismail Adamu, kwa jina lingine Athuman Mohamed Nyaubi (28), mfanyabiashara wa magari nchini Afrika Kusini na mkazi wa Morocco jijini Dar es Salaam.
Morine Amatus ni mkazi wa Mikocheni ‘B’ jijini Dar es Salaam na baba yake (Liyumba) alikuwa Mkurugenzi wa Utumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na aliwahi kufungwa miaka miwili, Mei 24, 2010 kwa makosa ya kutumia vibaya ofisi ya umma.
NZOWA ATAHADHARISHA
“Niwatahadharishe wale wote wanaofanya au kufikiria kufanya biashara hii haramu ya dawa za kulevya, waache kwa sababu polisi kwa kushirikiana na raia wema tumejipanga. Maeneo yote siku hizi tunayalinda, watakaojiingiza ni lazima watakamatwa tu,” alionya.
Kamanda Nzowa amewashukuru wote waliofanikisha kutoa taarifa ya kuwepo kwa madawa nchini na amewataka kuendelea kushirikiana na jeshi lake kwani alidai wote wanaokoa taifa na kuwa na watu mazezeta.