MBUNGE wa Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema), ameingia matatani baada ya kudaiwa kumtishia mtu kwa bastola katika kikao cha ndani cha chama hicho.
Wenje, ambaye amekanusha madai hayo, anadaiwa kufanya kitendo hicho katika mkutano wa Kamati ya Utendaji ya wilaya mbili za Nyamagana na Ilemela, Jumamosi, Mwanza chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.
Hata hivyo, alikiri jana kuwa na bastola kwenye mkutano huo akidai muda wote aliiweka kiunoni.
Wenje anadaiwa kufanya kitendo hicho kwa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Ilemela, Robert Gwanchele baada ya kushindwa kuelewana kikaoni.
“Katika purukushani hizo, Mbunge wa Viti Maalumu, ndiye aliyenusuru hali baada ya kuipiga kumbo silaha hiyo na kusababisha Wenje adondoke chini na kupata maumivu usoni, na mlengwa wa silaha hiyo kupata upenyo na kuchoropoka,” kilidai chanzo cha habari.
Wenje alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu tuhuma hizo jana, alikana kumtishia mtu kwa bastola kwenye mkutano huo na kuhusisha madai hayo na masuala ya migogoro ya kisiasa ndani ya chama hicho.
“Kwanza sikuwa na sababu yoyote ya kutishia mtu bastola ingawa kweli inawezekana ni peke yangu niliyekuwa na silaha hiyo kwenye mkutano huo … hakubishana nami sasa ningeanzia wapi? Yeye alibishana na Dk Slaa,” alidai Wenje.
Akisimulia tukio lilivyokuwa, Wenje alisema: “Ilikuwa Jumamosi kwenye kikao cha ndani cha chama kilichoongozwa na Dk Slaa, kabla hatujaanza, vijana wawili si wajumbe wa kikao waliingia, Dk Slaa akaamuru watoke, wa kwanza akatoka na wa pili akagoma.
“Aliyetoka kwanza ni Deus Litaragula wa Nyamagana na wa pili nilimtambua kwa jina moja la Gwanchere kutoka Ilemela, huyu aligoma kutoka, mimi nilikuwa nimekaa kwa mbele, watu wa nyuma alikokuwa huyu kijana wakaanza kumtoa kwa nguvu, ikazuka purukushani na kusukumana,” alisema Wenje.
Alidai kuwa alinyanyuka kwenda kusaidia kumtoa kijana huyo ili mkutano uendelee na kwa kuwa ilikuwa usiku, mtu wa kwanza kumtambua katika purukushani ya kumtoa nje kijana huyo ni Naibu Meya wa Mwanza, Charles Chibela.
Kwa mujibu wa Wenje, Litaragula kabla ya kupoteza sifa za kuhudhuria kikao cha Kamati ya Utendaji ya wilaya hizo mbili, alikuwa Katibu Mwenezi wa Chadema wa Wilaya ya Nyamagana, lakini hakujua nafasi ya Gwanchere.
“Kwa hali ya kawaida nisingeweza kutishia mtu ambaye sikubishana naye tangu awali, nilikwenda kusaidia kumtoa, hizo nyingine ni siasa, maana ni kikao kilichogusa migogoro ya kisiasa ndani ya chama na baadhi ya watuhumiwa ni hao waliotolewa, ndiyo maana nasema ni siasa,” alidai Wenje.
Kuhusu bastola Wenje alisema: “Kweli bastola nilikuwa nayo lakini sikumtishia nayo mtu yeyote, kwanza purukushani hiyo haikuhitaji hata kutumia rungu, sembuse bastola, nilikuwa nimevaa shati bila koti na nimekunja mikono labda katika harakati ilionekana na kudhaniwa natishia”.
Alidai wapo wanaoweza kusema, kwa kuwa aliyekuwa karibu ni Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia na meza kuu mbali ya Dk Slaa alikuwepo pia Katibu wa Mkoa wa Mwanza, Wilson Mushumbusi na Meya wa Jiji la Mwanza, Josephat Manyerere.
Dk. Slaa alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia tukio hilo alikataa kulizungumzia akidai kuwa analenga uchaguzi wa Arumeru Mashariki zaidi na kisha kukata simu.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alikiri kupata taarifa za suala hilo kwa njia ya mtandao na kueleza kuwa hatima yake itajulikana baada ya uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki na uchaguzi mdogo wa udiwani Kirumba, Mwanza.
“Ni kweli, tumelisikia hilo lakini akili na mawazo yetu yote sasa hivi tumeelekeza kwenye kampeni Arumeru na udiwani Mwanza, tukimaliza huko tutalishughulikia hilo. Lazima kusikiliza pande zote mbili na kuchunguza kila madai, kila kitu kina chanzo na huenda hata tukio lenyewe halipo jinsi linavyodaiwa,” alisema Mbowe.
Mbowe alifafanua, kuwa utaratibu wa chama hicho ni kutumia vikao na taarifa rasmi kuhusu tukio lolote na wakipata taarifa ya kilichotokea, watakaa na pande hizo mbili kulimaliza na ikibainika ukweli upo, watachukua hatua kwa mujibu wa utaratibu wao.
Alipoulizwa kwa taratibu zao endapo Wenje atakutwa na hatia watachukua hatua gani, Mbowe alisema: “Tusizungumzie kuvuka mto wakati bado hatujaona mto wenyewe, tuvute subira tutawaeleza kitakachojiri”.
Kutoka Mwanza, Grace Chilongola anaripoti kuwa Katibu wa Chadema wa Mkoa, Mushumbusi alisema tukio hilo halina ukweli bali ni uvumi ulioenezwa na mjumbe aliyeondolewa kwenye kikao hicho, baada ya kusimamishwa ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mkoa mwaka jana.
Kwa mujibu wa Mushumbusi, waliotolewa ni Litaragula, aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Nyamagana na Robert Gwanchere aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Ilemela, ambaye anadaiwa kueneza uvumi huo.
Katika hatua nyingine, Mbowe alipotakiwa kushauri kuhusu wimbi la matumizi holela ya silaha nchini, aliiomba Serikali kupitia Jeshi la Polisi kuzuia utoaji silaha holela kwa kuwa unahatarisha maisha ya watu badala yake vikosi vya ulinzi na usalama viimarishwe.
“Hatuwezi kuwa nchi ya watu wanaogawa silaha kama manati, mtu akipata umaarufu kidogo na vihela kidogo, anataka kumiliki silaha, ifike mahali tuelezwe ni Watanzania wangapi wanamiliki silaha na vigezo gani vinatumika kupewa hizo silaha, pia yapo mahitaji ya mafunzo ya matumizi ya silaha,” alisema Mbowe.
Alishauri wamiliki wa silaha kufuatiliwa kila wakati na kujua kama wanakumbuka matumizi ya silaha na kupunguza kutoa silaha kwa watu hata kama ni mamlaka iliyowekwa kisheria.
Wenje ni Mbunge wa pili kukumbwa na kadhia hiyo ya silaha baada ya Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM) kupanda jukwaani akiwa na bastola kiunoni kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni katika Jimbo la Igunga mwaka jana. Pia Dk. Slaa alipata kukutwa na silaha mkoani Arusha baada ya kupekuliwa katika gari alimokuwa.
0 Comments