ASKOFU wa Jimbo la Morogoro, Telesphor Mkude amesema ameshafanya uamuzi kuhusu padri wa kuongoza Parokia ya Lugoba mkoani Pwani, baada ya aliyekuwepo, Padri Philipo Mkude, kukataliwa na waumini.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dar es Salaam baada ya kuongoza Misa ya kuwabariki waumini wa Parokia ya Mbezi Luis kwa ujenzi wa kanisa, Askofu Mkude alisema alishafanya uamuzi tayari.
“Suala la Lugoba nilishafanya uamuzi tayari wa nani wa kuongoza ile Parokia na nimeacha viongozi wa ngazi nyingine kwa hatua ya utekelezaji, mimi nikipitisha jambo wengine ndiyo wanatekeleza,” alisema Askofu Mkude.
Alipoombwa kutaja jina la Padri atakayeongoza Parokia hiyo inayohudumiwa kiroho kwa zaidi ya mwezi mmoja na Parokia ya Chalinze, Askofu Mkude alisita na badala yake alimtaka mwandishi kuamini tu kuwa tayari uamuzi alishafanya.
“Nyie wenyewe ni mashahidi mmekuwa mkiandika na kufuatilia vizuri suala hili, binafsi naona ni busara kusubiri wale niliowakabidhi utekelezaji, watekeleze na mtaona tu kwamba mambo yamefanyika,” alifafanua.
Hata hivyo, wakati Askofu amedai kumaliza suala hilo, jana Misa katika Parokia ya Lugoba iliendelea kuongozwa na Paroko wa Chalinze, Chedi Mloka. Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilidai kuwa, Padri Mkude alifanya Misa asubuhi na Masista (Watawa wa Kike) wa parokia hiyo na kwamba makabidhiano ya padri mpya yanatarajiwa kufanyika siku yoyote wiki hii.
Jana Makamu wa Askofu, Padri Patrick Kung’alo hakupokea simu kuelezea hatua hiyo ya utekelezaji lakini mwishoni mwa wiki iliyopita alisema kuwa suala hilo limefikia hatua za mwisho.
Mgogoro baina ya waumini na Padri Mkude, ulijitokeza hadharani Februari 26, mwaka huu baada ya waumini zaidi ya 200 kuandamana hadi mbele ya lango la Kanisa wakiwa na mabango zaidi ya 20 yenye ujumbe wa kumkataa hali iliyosababisha kuzuia misa.
Walidai kuwa Padri huyo kwa nyakati tofauti kwenye mahubiri yake kanisani, amekuwa akiwatukana waumini wa Kabila la Wakwere wa parokia hiyo kuwa watoto wao ni wachafu, masikini, hawapeleki watoto shule, hawachimbi vyoo na wanacheza ngoma tu badala ya kufanya kazi za maendeleo.
Padre Mkude ambaye wiki hii mpaka jana alikuwa parokiani Lugoba, lakini bila kujihusisha na kutoa huduma kwa waumini, alipoulizwa alikana na kudai kuwa amekuwa akiwahamasisha kufanya kazi za maendeleo na kupeleka watoto shule, lakini wamekuwa hawamsikii na kubaki kucheza ngoma tu.
0 Comments