Skendo ya ngono inaitikisa Kanisa la Katoliki, Parokia ya Mburahati lililopo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na kusababisha mgawanyiko mkubwa kwa waumini.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu zimebaini kuwa skendo hiyo ya ngono inamhusisha Padri Paul Njoka na mhudumu wa nyumba za mapadri ambaye pia ni muumini wa kanisa hilo aliyejulikana kwa jina moja la Mwasiti.
Taarifa zilizopatikana kanisani hapo zinadai kwamba padri huyo alimjaza mimba mhudumu huyo na hivi sasa amezaa naye mtoto.
Habari hizo zilienea kanisani hapo na kusababisha baadhi ya waumini kutaka suala hilo liwekwe wazi ili kiongozi huyo achukuliwe hatua zaidi, jambo lililomfanya kasisi huyo atafute jinsi ya kujihami.
Chanzo chetu cha habari kinasema kwamba baadhi ya viongozi wa kanisa hilo walifikia hatua ya kutafuta jinsi ya kumficha mtoto huyo baada ya kuzaliwa ili kupoteza ushahidi.
Imeelezwa kwamba Februali 4, mwaka huu Padri Njoka akiwa na muumini aliyejulikana kwa jina la Maria Kaswela walichukua gari na kumsaka Mwasiti, walimpata na kumuingiza katika gari hilo.
Imedaiwa kwamba katika mzunguko wao, Mwasiti hakujua ni kitu gani alichotakiwa kufanyiwa na mtoto wake bali yeye alijua ni matembezi ya kawaida huku akifurahia ni jinsi gani padri anavyompenda mtoto wake na kuamua kuzunguka naye jijini kwa siku hiyo.
Chanzo kilidai kwamba siku hiyo padri huyo na mzazi mwenzake walielekea Sinza,Manzese kisha Magomeni.
MTOTO ATEKWA
Walipofika Magomeni habari zinasema walimtuma dukani mama wa mtoto (Mwasiti) na mtoto akawa amebebwa na Maria.


Chanzo kiliendelea kudai kwamba padri aliendesha gari na kuondoka eneo la Magomeni kwa kasi kuelekea kusikojulikana na Mwasiti alipotoka dukani na kwenda sehemu lilipoegeshwa gari hakuwaona na alipowapigia simu hawakupatikana.
TAARIFA YAFIKA POLISI
Hata hivyo, Mwasiti alipatwa na hofu kwani ilimchukua muda mrefu bila kuwaona, kitendo kichomfanya aende Kituo cha Polisi, Wilaya ya Kipolisi ya Magomeni kutoa taarifa ya kutekwa kwa mtoto wake wa siku 28 tangu azaliwe.

Mwasiti alifunguliwa jalada lenye kumbukumbu MG/RB/2430/2012 ndipo polisi walipoanza kazi ya kuwatafuta padri na Maria bila mafanikio.
Habari zinasema polisi walifanikiwa kumuona Padri Njoka akiwa kanisani siku ya Jumapili akiendesha ibada ila ilishindikana kumkamata kwa sababu misa ilikuwa ikiendelea.
Kutokanana kitendo cha padri huyo kuendesha misa, askari hao waliacha taarifa kwa mlinzi wa kanisa hilo kwamba baada ya kumaliza ibada afike Kituo cha Polisi Magomeni akiwa na Maria.
Hata hivyo, hawakwenda siku hiyo badala yake walienda kesho yake Jumatatu ya Februali 6, mwaka huu.
“Mara walipofika kituoni waliwekwa chini ya ulinzi, walibanwa ili waonyeshe alipo mtoto ambapo walisema kwamba yupo Kigamboni kwa ndugu wa padri huyo,” chanzo hicho kilisema.

Polisi waliwaamuru watoe namba ya simu ya watu walio na mtoto huyo ili wapigiwe, padri alitoa, ilipopigwa aliye na mtoto akaamriwa amlete kituoni hapo na akafanya hivyo saa 5.00 usiku padri akiwa chini ya ulinzi.
Hata hivyo, polisi walipomkabidhi Mwasiti mtoto wake alikataa kumpokea na kudai kwamba akapimwe afya yake kwanza kwa vile hakujua alichofanyiwa huko na alikua katika mazingira gani.
Chanzo kiliendelea kusema kwamba hapo polisi Magomeni alikuwepo pia Paroko Timoth Nyasulu Maganga ambaye ni mkubwa wake wa kazi Padri Njoka.
Habari zinasema Padri Maganga alimbembeleza Mwasiti amchukue mtoto wake ambaye alikubali kisha alikwenda naye Kinondoni kwa dada wa mzazi huyo. Uchunguzi wetu umebaini kuwa kesi hiyo ipo chini ya mpelelezi mwenye namba WP697 Tiba.
WARAKA KWA PENGO
Kutokana na kitendo hicho, baadhi ya waumini wa kanisa hilo waliamua kumuandikia barua Februali 8, mwaka huu Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Muadhama Askofu Polycarp Kadinali Pengo kuhusu udhalilishaji wa Kanisa Katoliki waliodai kufanywa na padri huyo kwa kumteka mtoto.

Katika barua hiyo (Nakala tunayo) waumini hao wameeleza jinsi wachunga kondoo walivyofikia hatua ya kufanya mapenzi na wafanyakazi, wahudumu wa nyumba ya mapadri na kuwapa mimba
Hata hivyo, katika barua hiyo waumini hao wamesikitishwa na kitendo hicho na kudai kuwa gharama kubwa za fedha za kanisa zimetumika kushughulikia suala hilo.
“Tunakuomba ufanyie kazi jambo hili kwa haraka inawezekanavyo ili kuepusha uvunjifu wa amani endapo viongozi hao wachafu watabaki hapo parokiani,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo imeendelea kueleza kuwa mapenzi yanayofanyika kanisani hapo kati ya viongozi na waumini yamesababisha utoaji hovyo wa mimba hadi wengine kuzalishwa, kitendo ambacho kinalitia aibu Kanisa Katoliki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela hakupatikana kuzungumzia tukio hilo lakini afisa mmoja wa cheo cha juu wa jeshi hilo alithibitisha kuwepo kwa madai hayo kuongeza kuwa upelelezi bado unaendelea.

Aidha, Kadinali Pengo hakuweza kupatikana kuzungumzia malalamiko hayo ya waumini wake.