Stephen Wassira |
Pamoja na kuliangukia Kanisa, bado Wassira ameendelea kushikilia msimamo wake wa kumtaka Dk. Slaa ajitokeze mbele ya Watanzania ili kuweka wazi sababu iliyomfanya kuvunja nadhiri ya upadri na kukimbilia siasa.
Akizungumza na viongozi wa CCM, wa dini na wananchi katika mkutano wa ndani Usa River
jana, Wassira alisema katika maisha yake amekuwa akiliheshimu Kanisa Katoliki na viongozi wake na kwamba viongozi hao wanalijua hilo.
"Naliheshimu sana Kanisa Katoliki na madhehebu yote. Naheshimu Katiba ya Nchi inayoruhusu uhuru wa kuabudu, sitaki malumbano na Kanisa hilo, Slaa alikuwa Padri kuna
habari kwamba alikula sadaka, naomba ajitokeze yeye mwenyewe ajibu tuhuma hizi ili tujue ukweli ni upi, asiwaambie Kanisa wajibu ili kutaka kunigombanisha na Kanisa," alisema Wassira.
Alisema Kanisa Katoliki lina taratibu zake za kushughulikia masuala yao na kamwe si jambo jema kuliingilia katika taratibu hizo lakini kwa vile Dk. Slaa ni kiongozi wa kijamii aliyepata kuwania hata urais wa nchi, ni vema akajisafisha dhidi ya tuhuma ya kulikosea Kanisa Katoliki hatua iliyomfanya aondolewe kwenye huduma hiyo.
"Mimi ni Mkristo, natambua taratibu za Kanisa. Ukiwa umetenda dhambi unakwenda kwa Padri na kutubu na yeye wala Kanisa hawaji katika jamii kutangaza ulichokifanya. Slaa alivunja nadhiri na Yesu, akaacha upadri ni vizuri akajibu mwenyewe, maana ni kiongozi katika jamii pana," alisema.
Pamoja na hilo, Wassira alisema viongozi wa dini wana wajibu wa kukemea uvunjifu wa amani unaofanywa na baadhi ya vyama vya siasa nchini, ili kuliokoa Taifa na kutumbukia katika machafuko yanayoweza kusababisha maafa makubwa mbeleni.
CCM na mafisadi
Katika hatua nyingine, Wassira alizungumzia madai yanayotolewa na Chadema kwamba CCM ni chama cha mafisadi, akisema madai hayo si ya kweli kwa vile si wan chama wote wa CCM ni mafisadi. "Slaa aje hapa anieleze mimi Wassira nilifisadi nini, alete ushahidi.
CCM ni chama chenye wanachama milioni tano, akisema ni chama cha mafisadi ana maana nyie nyote hapa ni mafisadi.
Hakiwezi kuwa chama chote cha mafisadi, lakini wapo baadhi ya wana CCM ambao wamepotoka kutokana na mambo ya ubinadamu.
"Mimi Wassira naweza kufanya makosa ndani ya CCM, kinachofanyika ni kwa chama kunionya na baada ya hapo lazima kisonge mbele. CCM haiwezi kushindwa kuongoza Watanzania kwa vile eti kuna wachache wanajihusisha na ufisadi. Hata katika madhehebu ya dini anapopotoka
Shehe au Padri anachukuliwa hatua, lakini ibada zinaendelea," alisema.
Alisema wananchi wa Arumeru Mashariki wana wajibu wa kuichagua CCM kutokana na kuwa na mifano hai ya vurugu zinazosababishwa na vyama vya upinzani katika Arusha Mjini, hatua ambayo imechafua sifa ya mji huo.
"Arusha zamani ilikuwa inaitwa Geneva ya Afrika, lakini sasa sifa hiyo haipo tena. Zamani watalii na wageni walikuwa wanakuja na KLM (Shirika la Ndege la Uholanzi) wanatua KIA
(Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro), halafu wanakwenda Arusha, lakini sasa wanakuja hawashuki KIA wanakwenda Zanzibar kutokana na fujo."
Alisema ushindi wa Chadema Arusha Mjini ulitokana na mgawanyiko wana CCM katika kura za maoni, lakini katika hali ya kawaida, wasingeshinda kwa vile CCM ina wanachama, wafuasi na
mashabiki wengi kuliko chama kingine chochote Arusha.
Polisi yaonya
Kwa upande mwingine, Jeshi la Polisi nchini limevionya CCM na Chadema kuacha kutumia lugha ya uchochezi majukwaani na pia kuacha kulifundisha Jeshi hilo namna ya kufanya
kazi.
Kamishina Msaidizi wa Polisi, Isaya Mngulu ambaye ni Mkuu wa Operesheni ya uchaguzi Arumeru Mashariki kwa Jeshi hilo, alisema polisi haitavumilia kuona viongozi wa vyama vya siasa wanaendesha kampeni zitakazosababisha vurugu na kuondoa amani na utulivu uliopo.
Alitolea mfano wa kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Martin Shigela hivi karibuni, kwamba chama hicho kitawaagiza wafuasi wake kuingia msituni kama polisi watashindwa kufanya kazi yao ipasavyo, kwamba ni lugha ya uchochezi.
Kwa upande wa Chadema alisema kauli ya Dk. Slaa kwamba Polisi haijawakamata watu wanaodaiwa kusababisha vurugu katika mikutano ya kampeni kwa vile ni wanachama wa CCM, pia inachochea uvunjifu wa amani kwani unaweza kuwafanya watu kujichukulia sheria mikononi.
Alisema Jeshi la Polisi litaendelea kufanya kazi zake kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria, ili kuhakikisha vyama vyote vinashiriki uchaguzi mdogo wa ubunge katika hali ya amani na utulivu.
Nyangwine aibuka Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine, alisema amelazimika kukatisha ziara ya kulitembelea jimbo lake ili kuja Arumeru kuwaeleza wananchi namna wilaya ya Tarime ilivyozorota kimaendeleo kwa miaka mitano tangu mwaka 2005 kutokana na kuichagua Chadema.
Alitoa siri kwamba Dk. Slaa aliumbuka katika uchaguzi wa ubunge mwaka 2010 pale alipochapisha fulana zilizoandikwa 'Mambo Kama Tarime' akiamini Chadema ingeshinda
uchaguzi huo na kuzitawanya fulana hizo nchi nzima, lakini badala yake wananchi waliichagua CCM.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu tangu CCM ilipolitwaa Jimbo hilo la Tarime kumekuwa na maendeleo makubwa kutokana na hali ya amani na utulivu hatua inayowafanya wananchi kujishughulisha na maendeleo zaidi na si maandamano kama ilivyokuwa awali.
Aliwataka wananchi wa Arumeru kuchagua mgombea wa CCM, Sioi Sumari, akiahidi kushirikiana nao kwa kuwasambazia vitabu vya kufundishia shule za sekondari kama ambavyo amekuwa akifanya katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kukuza elimu na kuharakisha
maendeleo.
Alisema vurugu za Tarime hivi sasa zimehamia Musoma Mjini, iliyoko chini ya Mbunge wa Chadema, Vincent Nyerere, hatua ambayo imelifanya jimbo hilo kuanza kudorora kimaendeleo na wananchi kuhusika na vurugu na maandamano yasiyo na msingi.
Maji Marefu
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani ‘Profesa Maji Marefu’
alieleza kushangazwa na hatua ya baadhi ya magazeti ya jana (si gazeti hili) kuchapisha picha inayomwonesha akiwa na mgombea ubunge wa Chadema, Joshua Nassari na Meneja wake wa Kampeni, Vincent, wakifurahi pamoja wakati hajawahi kupiga picha kama hiyo.
Alisema anachokumbuka yeye ni kwamba juzi alikwenda katika kambi ya Chadema Usa River, kuwasalimia wabunge wenzake wa CCM na alipiga picha ya pamoja na Vincent na mtu mwingine aliyegombea naye ubunge Korogwe Vijijini, lakini katika picha hiyo Nassari hakuwapo.
"Nashangaa kuona ile picha eti nafurahi na Nassari wakati si kweli, kwani Nassari yeye alipofika alinifanyia fujo na kunitishia na niliokolewa na wabunge wenzangu maana ilikuwa ni hatari sana, lakini nilishangaa jana kuona picha nafurahi pamoja naye," alisema Ngonyani.
Aliwataka wananchi kuwapuuza Chadema na kuichagua CCM katika uchaguzi huo wa Aprili mosi.
0 Comments