Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) Tido Mhando
ASEMA ATAONGEZA UBORA WA HABARI NA KUKUZA DEMOKRASIA
Kizitto Noya
BODI ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), imemteua mwandishi wa habari mkongwe barani Afrika, Dunstan Tido Mhando, kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa kampuni hiyo.Tido alianza kazi rasmi jana, muda mfupi baada ya kumalizika kwa hafla ya kumkaribisha, iliyofanyika katika ofisi za kampuni hiyo zilizoko Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

Tido anachukua nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Sam Shollei ambaye mkataba wake wa kazi ulimalizika mwishoni mwa mwaka jana. Shollei kwa sasa ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Nation Media Group (NMG)

Kabla ya kujiunga na MCL, Tido alishafanya kazi ya uandishi wa habari ndani na nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 30.
Amewahi kufanyakazi katika iliyokuwa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kisha kwenda nje ya nchi na kufanikiwa kupata heshima ya kuwa Mwafrika wa kwanza, kuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC). Akiwa BBC, Tido aliingia katika historia ya habari kwa kuwa mwandishi wa habari ambaye amefanya mahojiano ya ana kwa ana marais wengi wa Afrika.

Mbali na BBC, Tido amewahi pia kufanya kazi katika mashirika mengine ya habari ya nje ambayo ni pamoja na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VoA) na Redio Deutche Welle (DW) ya Ujerumani.

Akizungumza ofisini kwake Tabata Relini jana, Tido alisema: "Ninafurahi kujiunga na kampuni ya Mwananchi na nitatumia uzoefu wangu kuiinua kampuni kwa kuongeza kiwango cha weledi wa habari."

Kuhusu historia yake, Tido alisema alianza kazi ya uandishi wa habari mwaka 1969 Redio Tanzania, akiwa mtangazaji, akabobea hasa katika michezo, hasa mpira wa miguu.

"Niliwahi kutangaza mpira katika nchi nyingi ikiwamo Uganda katika Kombe la Chalenji mwaka 1973, mashindano ya Nchi za Jumuiya ya Madola mwaka 1974 na nilikuwa nasafiri na Taifa Stars katika nchi kadhaa ikiwamo Nigeria, Sudan, Kenya na Malawi," alisema Tido.

Wakati akiripoti kwenye Michezo ya Madola huko Christchurch, New Zealand mwaka 1974, Tido alikuwa shuhuda wakati mwanariadha wa Tanzania, Filbert Bayi alipovunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500 alipomsambaratisha bingwa wa dunia wa wakati huo.

"Mwaka 1976 nilichaguliwa kwenda kutangaza mashindano ya Olimpiki nchini Canada, ingawa Tanzania ilijitoa na mwaka 1978 nilienda kutangaza mashindano ya nchi za Jumuiya za Madola huko Edmonton, Canada, kabla sijaenda nchini Kenya mwaka 1979 kutangaza mechi za Kombe la Chalenji na Taifa Stars."

Katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 1978 nchini Canada, Tido alitangaza moja kwa moja wakati Mtanzania Gidamis Shahanga alipotwaa medali ya dhahabu kwenye marathon na Bayi alipata medali ya fedha kwenye mbio za mita 1500.Tido alisema baada ya mashindano hayo, alichukuliwa na kampuni ya High Fidelity Production Ltd ya nchini Kenya akiwa mtengenezaji wa vipindi na baadaye kuanza kufanya kazi ya uandishi wa habari kwa kujitegemea akiyawakilisha mashirika ya BBC, VoA na Dutch Welle.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communication, Profesa Palamagamba Kabudi akimkaribisha ofisini Mkurugenzi Mtendaji mpya wa MCL Tido Mhando, katikati ni Mhariri Mtendaji wa kampuni hiyo Theophil Makunga
Nilikaa Kenya kwa miaka kumi kuanzia 1980 hadi 1990, wakati huo nikiwa mwakilishi wa mashirika hayo katika nchi zote za Afrika Mashiriki na Kati. Moja ya habari maarufu nilizowahi kutangza nikiwa Kenya, ni ile ya kuibua taarifa ya kifo cha kutatanisha cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Dr Robert Ouko kunako mwaka 1990," alisema Tido.

Tido alisema mwaka 1990 hadi 2007, alijiunga na BBC na anajivunia kuwa Mwafrika wa kwanza kuliongoza shirika hilo katika Idhaa ya Kiswahili na kufanikiwa kuongeza idadi ya wasikilizaji kutoka milioni saba hadi milioni 21 kwa juma."Ilipofika mwaka 2007, Rais Jakaya Kikwete alinifuata London, Uingereza, na akanitaka nirudi nchini kuliongoza Shirika la Habari la Taifa (TBC)," alisema, na kuongeza:
"Ninafurahi kuja Mwananchi, kampuni kubwa ya habari nchini na nitatumia uzoefu wangu kutoa mchango wangu katika kukuza demokrasia ya kweli nchini kwa faida ya Watanzania na taifa kwa ujumla."

Akizungumzia ujio wa Tido, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Theophil Makunga, alisema kampuni ya Mwananchi ina kila sababu ya kufurahia kumpata mkurugenzi huyo mpya kwani atasaidia kuharakisha mafanikio ya kampuni.

"Tumepata mtu makini na mwenye msimamo katika taaluma ya habari na tunaamini atatusaidia sana. Hakika tumempata mtu sahihi kwa wakati sahihi," alisema Makunga.