Khatimu Naheka na Wilbert Moland
HALI ya joto la Dar es Salaam imeonekana kuwatesa wachezaji na msafara mzima wa kikosi cha ES Setif ya Algeria ambao wamelalamika kuwa wanapata tabu kutokana na hali hiyo.
Kikosi hicho kilichotua juzi jijini kwa ajili ya kuivaa Simba katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, utakaopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, jana kilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume huku wachezaji wakinywa maji mara kwa mara.
Katika mazoezi hayo, baadhi ya wachezaji wa timu hiyo walicheza wakiwa vifua wazi huku wakiwa wanasimamisha mazoezi na kujimwagia maji na wengine kunywa kila baada ya dakika 10.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Geiger Alain, 52, raia wa Switzerland, alisema hali ya joto inawapa tabu wachezaji wake ambao walionekana kuchoka kwa haraka katika mazoezi.
“Tulifika salama lakini joto ni kali sana jambo ambalo limeonekana kuwapa shida wachezaji wangu, tulifanya vizuri kufika mapema kwa kuwa naamini watazoea haraka,” alisema kocha huyo.
0 Comments