Mwenyekiti wa taasisi ya Muttie Mengi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi (aliyemshika mtoto), wanachama wa Klabu ya Lions ya Dar es Salaam (Host) wakiwa katika picha ya pamoja Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere na watoto wenye matatizo ya moyo, mwishoni mwa wiki baada ya watoto hao kurejea kutoka nchini India.
Wagonjwa 21 wa moyo waliokwenda nchini India kwa upasuaji wamerejea nchini wakiwa na afya njema.
Waliwasili juzi jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kulakiwa na viongozi wa klabu ya Lions ya Dar es Salaam (host) na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwapokea wagonjwa hao, Mengi aliwashukuru viongozi wa Lions, Shiraz Rashid na Mwenyekiti wa hospitali ya Regency, Dk. Rajni Kanabar, kwa namna wanavyotumia muda wao mwingi kuratibu safari za wagonjwa hao.
Alisema mara nyingi watu wanadhani msaada lazima uwe wa fedha tu wakati watu wanaojitolea muda wao kama viongozi hao wa Lions wamekuwa na msaada mkubwa sana katika kusaidia wagonjwa hao.
“Hivi karibuni nilisema kwamba sisi Wakristu tunaamini kuwa mali zote tulizonazo ni za Bwana, nikasema sitafilisika kamwe, lakini watu walitafsiri kwamba najivuna, ukweli ni kwamba kama unaamini mali zote ulizonazo ni za Bwana basi wewe ni maskini,” alisema.
Mratibu wa maradhi ya moyo katika klabu ya Lions, Dk. Kanabar, alipongeza taasisi ya Rodney Mutie Mengi Foundation, kupitia Mengi, kwa kusaidia mara kwa mara wagonjwa wanapokwenda India kwa matibabu.
Alisema miongoni mwa wagonjwa hao yumo mtoto wa miezi saba, Sinani Maliha Makame, ambaye baada ya upasuaji ameanza kuongezeka uzito baada ya tundu lake lamoyo kuzibwa kitaalam.
“Tunawashukuru wataalam wote wa Fortis Escorts Heart Institute kwa kutoa punguzo la Dola 2,000 kwa upasuaji wa kila mgonjwa anayetoka Tanzania, Wizara ya Afya ya Zanzibar, Mengi, kwa kutoa Dola 20,000 kwa upasuaji wa wagonjwa 10 katika ahadi yake ya kupeleka nje wagonjwa 50 wa moyo wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya uhuru na Regency kwa kuratibu safari,” alisema.