KATIKA hali isiyo ya kawaida, wanafunzi saba wa kidato cha nne katika Sekondari ya Mahida wilayani hapa, wamepata ujauzito katika kipindi cha miezi mitatu.

Aidha, imebainika licha ya tatizo la mimba, shule hiyo imekithiri kwa vitendo vya kihuni na uhalifu, vikiwamo vya utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya.

Hayo yalifichuka juzi kwenye kikao cha wazazi shuleni hapo, ambapo baadhi ya wazazi waliujia juu uongozi wa shule na kuutupia lawama kuwa ndio chanzo cha balaa hilo, kwa kuwa umeshindwa kutimiza majukumu ya kulea wanafunzi katika maadili mema.

Walisema katika mazingira kama hayo, haishangazi kuona katika kipindi cha miaka mitano mfululizo, matokeo ya kidato cha nne kwa shule hiyo ni mabaya, huku wakisisitiza kuwa hali hiyo inachangiwa na walimu kushindwa kusimamia taaluma.

“Hili ni jambo la aibu kwa shule kama hii wanafunzi kujihusisha na uuzaji bangi tena wanafunzi wa kike ndio wanafanya biashara hiyo, Mwalimu Mkuu na wenzake wanakuwa wapi?
Wanafunzi wanaongoza kwa kufeli na walimu wanaona kawaida tu. Tunaomba walimu wa shule hii wachukuliwe hatua,” alisema mmoja wa wazazi hao. Mzazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Baltazar Morris alisema matokeo ya uuzaji dawa za kulevya ni pamoja na kufanya ujambazi mitaani na ngono zembe zinazosababisha ongezeko la mimba za utotoni, kwani huuziana dawa hizo wenyewe kwa wenyewe.



Aliongeza kuwa, vitendo hivyo vya aibu vinaipotezea shule hiyo sifa na kinachosikitisha ni kuona wanafunzi wakifanya mambo hayo wakiwa shuleni, lakini nyumbani hawaoneshi dalili za kwenda kinyume cha maadili ya jamii.

Akijibu tuhuma hizo, Mkuu wa Shule, Henry Massawe alikiri kuwapo ongezeko la mimba na kudai kuwa kati ya Januari na Machi wanafunzi hao saba wa kidato cha nne walibainika kuwa na ujauzito.

Massawe alisema lawama wanazotupiwa walimu si sahihi, kwani kazi ya kulea watoto hao ni ya pande zote mbili wanapokuwa shuleni na wanapokuwa nyumbani. Alisema badala ya wazazi hao kuwanyooshea vidole walimu, ni vyema wakaanza kufuatilia nyendo za watoto wao na ikiwa ni pamoja na kuangalia maendeleo yao kitaaluma.

“Wanafunzi wa hapa wanaishi majumbani, wanakuja shuleni asubuhi na wanarudi nyumbani jioni baada ya masomo, hivyo wazazi wachukue nafasi yao kama wazazi, waache kulaumu walimu, vitendo hivyo vinaweza kudhibitiwa kama wazazi watashirikiana na walimu,” alisema Massawe.