MAHAKAMA ya Wilaya ya Sumbawanga imemhukumu mkazi wa Kijiji cha Kawila wilayani humo, Steven Kacheza, kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kumtia hatiani kwa unyang'anyi wa kutumia silaha.
Hakimu Adamu Mwanjokolo ametoa hukumu hiyo mwishoni mwa wiki baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi Millah Mgimwa.
Awali mwendesha mashitaka huyo aliieleza Mahakama kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 19, mwaka jana saa 2 usiku katika Kijiji cha Kipeta Sumbawanga Vijijini, ambako aliweka kizuizi cha magogo barabarani na kusababisha mwendesha pikipiki aliyefahamika kwa jina la Uchura Haonga kudondoka.
Ilidaiwa na Mwendesha Mashtaka huyo kuwa baada ya kudondoka, walijitokeza watu wawili ambao walikuwa na silaha alizozitaja kuwa bastola, panga na fimbo ambapo walimpiga mwendesha pikipiki huyo kisha kumnyang'anya pikipiki hiyo, fedha taslimu Sh 104,000 na simu aina ya Nokia.
Mgimwa aliieleza Mahakama kuwa baada ya taarifa kufikishwa Polisi, msako mkali ulifanyika ambapo Julai 21 saa moja asubuhi, mtuhumiwa alikamatwa akiwa na pikipiki hiyo aliyoipeleka kwa fundi kwa matengenezo.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mwanjokolo alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ambao ulileta mashahidi wanne akiwamo mmiliki wa pikipiki hiyo na askari waliomkamata mtuhumiwa huyo, hivyo alimhukumu mshitakiwa huyo kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30
0 Comments