Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) akiondoka kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha baada ya kusikiliza hukumu yake ambapo mahakama hiyo ilitengua matokeo ya uchaguzi uliopita na kumvua ubunge jijini humo. (Picha na Marc Nkwame).

BAADA ya Mahakama Kuu ya Arusha kumvua ubunge Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema (Chadema), kiongozi huyo amesema hatakata rufaa kwa kuwa hataki kuwa mbunge wa rufaa.

Jana Jaji Mfawidhi Kanda ya Sumbawanga, Gabriel Rwakibarila, alimvua ubunge Lema katika hukumu ya kesi iliyokuwa ikimkabili ya kupinga matokeo ya uchaguzi uliompa ubunge.

Hukumu kwa Lema Jaji Rwakibarila katika hukumu hiyo, alitaja sababu kuu nane zilizomshawishi kutengua ubunge wa Lema, zikiwamo za kutoa matusi, kashfa na kejeli katika mikutano ya kampeni.

Alisema kanuni, taratibu na Sheria ya Maadili ya Uchaguzi ya Mwaka 2010, zinakataza mgombea kutoa lugha za matusi, kashfa na kejeli na Lema alifanya hivyo huku akijua kuwa ni kinyume cha sheria.

Hoja zilizotupwa Rwakibarila alisema katika hoja kumi zilizowasilishwa mahakamani na mawakili wa wanachama watatu wa CCM waliofungua kesi hiyo, Alute Mughwai na Modest Akida, alitupilia mbali hoja mbili tu. 
Alizitaja kuwa ni madai kuwa Lema katika kampeni aliwataka wananchi kutochagua mgombea wa CCM, Dk. Batilda Buriani, kwa kuwa ni mkazi wa Zanzibar, hivyo hastahili kupewa ubunge Arusha Mjini.

Jaji Rwakibarila alisema hoja hiyo haina mashiko, kwa kuwa kusema Dk. Batilda ni mkazi wa Zanzibar haina maana ya kashfa.



Hoja nyingine aliyotupilia mbali ni ya udini, ambapo ilidaiwa kuwa Lema katika mikutano yake ya kampeni alisema Dk. Batilda asichaguliwe kwani anavaa kilemba ni Al Qaeda na pia atafunga Radio Safina na kujenga Msikiti .

Jaji alisema hoja hiyo nayo haina mashiko, kwani kuvaa kilemba si kuwa Al Qaeda kwani wako wanawake wengi wanavaa vilemba na pia hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa atafunga redio hiyo na kujenga Msikiti.

Hoja zilizombana Lema Katika moja ya hoja zilizoungwa mkono na Jaji Rwakibarila, ni pamoja na ya Lema kuthibitika kutumia kashfa, kejeli na udhalilishaji katika mikutano yake.

Kashfa hizo kwa mujibu wa Jaji Rwakibarila, ni kauli za Lema kuwa Dk. Batilda ni hawara wa mzee wa Monduli na kwamba ana mimba ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa. 
Hoja nyingine ni kauli ya Lema katika mikutano yake akiwataka wananchi kutomchagua Dk. Batilda kwa sababu ni mwanamke, ambapo Jaji Rwakibarila aliita kauli hiyo kuwa ni ya ubaguzi wa kijinsia.

Tume iambiwe Kutokana na sababu hizo, Jaji aliamua kutengua ubunge wa Lema na kumtaka Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, George Hubert, aiarifu rasmi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mara moja kuhusu uamuzi huo na kumwagiza Lema alipe gharama za kesi hiyo.

Taharuki mahakamani Lema hakuwa tayari kuzungumza na waandishi mahakamani hapo kama kawaida yake, bali aliondoka kwa miguu umbali wa meta 400 na gari lake lilimfuata.

Awali saa 1.30 asubuhi, viwanja vya ndani vya Mahakama Kuu vilitawaliwa na ulinzi mkali wa askari kanzu na wenye sare na askari wa mbwa na kuruhusu watu maalumu kuingia ndani ya Mahakama hiyo kusikiliza hukumu.

Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, George Hurbert, alifanya kazi ya ziada ya kukodi vipaza sauti na kuviweka nje ya Mahakama, ili kuwapa fursa watu kusikiliza wakiwa hata umbali wa meta 300.

Hukumu hiyo kwanza ilisomwa kwa Kiingereza na kufanya baadhi ya watu kukaa kimya wasielewe kinachoendelea na Jaji aliporudia kwa Kiswahili kwa faida ya wengi, ndipo sauti za vilio zilisikika kutoka kwa wanawake, vijana na wazee huku wakisema haki haikutendeka!  
Vilio hivyo vilivyodumu kwa zaidi ya dakika 30 vilifanya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia kukaa tayari kwa lolote, hali iliyofanya wafuasi wa Chadema kutawanyika kwa amani. Mitaani Katika vijiwe vya Chadema vya Soko Kuu la Arusha, Stendi Kuu ya Mabasi, vijiwe vya kuuza na kununua madini vya mtaa wa Pangani na St Thomas vilikuwa kimya na watu wachache tu wakijadili hukumu hiyo.

Akizungumzia uamuzi huo, Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, alisema akiwa kiongozi wa Arusha, haoni sababu ya kukata rufaa, bali kujiandaa na kuingia kikamilifu katika uchaguzi wa pili wa marudio.


Mwigamba alisema kukata rufaa ni kupoteza muda kwani kinachotakiwa ni kujiandaa kikamilifu kuiangusha tena CCM kwa kura nyingi tofauti na zilizopita.