WAKATI Watanzania katika maeneo mengi wakilalamikia ukosefu wa dawa, imebainika kuwa dawa zenye thamani ya Sh bilioni 4.7 zilizonunuliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zimeharibika.
Wabunge wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) wamehoji dawa hizo za thamani kubwa hivyo kuharibika wakati wananchi wakikosa dawa kwenye zahanati nyingi hasa vijijini.
Eneo lingine ambalo wabunge wamehoji ni kiasi kikubwa cha fedha zinazochukuliwa na Mamlaka ya Dawa na Chakula (TFDA) wakati inapokagua dawa zilizoagizwa na Serikali.
Kamati hiyo ilielezwa jana Dar es Salaam, kuwa TFDA inatoza asilimia mbili ya thamani ya dawa zinazonunuliwa na Serikali au zinazotolewa na wahisani hali iliyosababisha Bohari ya Dawa (MSD) kuwa na deni la Sh bilioni 45.
Kwa nini TFDA itoze Wizara mama fedha nyingi kiasi hiki, hivi kweli wanastahili kulipwa Sh bilioni 4 kwa kuchunguza dawa zinazoingia nchini, ni kitu gani kinafanywa na Mamlaka hii?” alihoji John Chenyo ambaye ni Mwenyekiti wa PAC na Mbunge wa Bariadi Mashariki.
Cheyo aliongeza kuwa Sheria inayoipa TFDA kutoza kiasi hicho cha fedha ni mbovu; kwani gharama zinazolipwa na Serikali kwa Mamlaka hiyo, mzigo wake unakwenda kwa wagonjwa. Alisema: ”TFDA ni watoa huduma si wafanyabiashara kama wanavyoonekana hapa.”
Eneo lingine ambalo rekodi za Wizara hiyo haziko sawa ni ununuzi wa gari la Waziri aina ya Toyota Land Cruiser V8 ambalo ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonesha kuwa gari hilo limenunuliwa kwa Sh milioni 191; bei ambayo iliwashitua wabunge.
Lakini Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilieleza kuwa ilinunua gari hilo kwa fedha zisizozidi Sh milioni 90 jambo ambalo wabunge walitaka rekodi sahihi zioneshwe.
“Sh milioni 90 ununue V8! Hilo gari limetengenezwa Manzese? Hapa kuna tatizo,” alisema Cheyo.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Regina Kikuli akitoa maelezo alisema chanzo cha dawa kumaliza muda wake bila matumizi, ni wahisani kuleta dawa ambazo wakati mwingine zimeshanunuliwa na Serikali.
Lakini alisema wameanzisha mpango ambao utasaidia kufanya wahisani walete dawa nchini kwa mikataba kulingana na kiasi cha dawa kilichoko nchini.
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Donan Mmbando, aliongeza kuwa kuharibika kwa dawa hizo kulitokana pia na tabia ya Serikali kupeleka dawa katika maeneo ambako hazistahili.
Wakati huo huo, Dk. Mmbando alisema Serikali imeshanunua pikipiki za matairi –bajaj- 372 ambazo walizisambaza vijijini. Alisema hawajapokea malalamiko ya matatizo ya pikipiki hizo na kwamba Serikali haiwezi kununua zingine hadi ifanye tathmini.
Alitoa maelezo hayo baada ya wabunge kutaka kujua mpango huo uliotangazwa na Serikali utekelezaji wake umefikia wapi.
0 Comments