Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma itatoa hukumu ya kesi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), Aprili 27, mwaka huu 2012 baada ya kukamilika kwa ushahidi wa pande zote.

Jaji Moses Mzuna wa Mahakama Kuu Kanda ya Kilimanjaro aliyeisikiliza kesi hiyo, alisema jana mjini hapa kuwa baada ya majumuisho hayo, atatoa hukumu siku hiyo.

Jumla ya mashahidi 24 wa upande wa walalamikaji walitoa ushahidi wao na upande wa walalamikiwa walikuwa mashahidi watatu.

“Nawashukuru sana wote mlioshiriki kwa namna zote katika kesi hii, kila upande umejitahidi kuisaidia mahakama, sasa hukumu itakuwa tarehe 27, mwezi huu,” alisema Jaji Mzuna.

Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Machi 12, mwaka huu, imefunguliwa na wanchama wawili wa CCM Shabani Selema Itambu na Pascal Masele Hallu, wakazi wa kijiji cha Makiungu, wilayani Singida.

Wanachama hao wanapinga matokeo yaliyompa ushindi Lissu kuwa mbunge wa wa Singida Mshariki kwa madai kuwa taratibu za uchaguzi zilikiukwa.

Katika kesi hiyo, pia Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wameunganishwa.

Lissu alitangazwa mshindi katika uchaguzi huo wa Oktoba 2010 dhidi ya aliyekuwa mgombea kupitia CCM, Jonathan Njau.

Wadai wanatetewa na wakili Godfrey Wasonga, wa kampuni ya Wasonga $ Associates Advocates ya Dodoma na Lissu alisimama mwenyewe akishirikiana na wanasheria watatu walioongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Vincent Tangoh.