Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Palette Media Co Ltd, Redemptus Masanja (kulia) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu uzinduzi wa kipindi cha television cha ‘Mwana Dar es Salaam unaotarajiwa kufanyika Aprili 28 mwaka huu jijini humo. Katikati ni Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya PBZ, Juma Hafidh ambao ni wadhamini wakuu wa uzinduzi huo na kushoto ni Qamara Slani Joseph,Meneja Mahusiano ya Jamii wa kampuni ya Palette Media.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KIPINDI CHA LUNINGA CHA ‘MWANA DAR ES SALAAM’ KUZINDULIWA JIJINI DAR ES SALAAMDar es Salaam 23 April, 2012. KIPINDI cha television cha ‘Mwana Dar es Salaam’ kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam tarehe 28 April mwaka huu katika hafla itakayofanyika katika ukumbi wa Dar Live jijini humo.
Kipindi cha television cha ‘Mwana Dar es Salaam’ ambacho kitakuwa kikibeba masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa kitafanya uchambuzi wa kina katika matukio mbalimbali yaliyotokea ama yanayoendelea kutokea nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Palette Media Co Ltd, Redemptus Masanja ambao ni waandaaji wa kipindi hicho amesema jijini Dar es Salaam leo katika kipindi hicho kitakachokuwa kikirushwa hewani na kituo cha television cha Clouds TV, kitaibua matukio muhimu yaliyotokea nchini kuhusu Mali, Maisha ya Watu, Majanga ya aina mbalimbali na Rasilimali za Taifa na katika kufanya hivyo kusaidia juhudi za kutafuta suluhisho la kudumu.
Uzoefu unaonyesha kuwa mara kwa mara matukio mbalimbali yanapotokea hususani matukio ya ajali juhudi nyingi huchukuliwa na serikali na mamlaka mbalimbali husika hivyo kampuni ya Palette Media imeona kuna haja ya kuanzisha kipindi hiki ili kuunga mkono juhudi hizo si kwa lengo la kukosoa au kulaumu bali ni katika kutafuta mbinu ili kujaribu ama kuyazuia au yasitokee tena na kama yakitokea basi ni hatua gani zinapaswa kuchukuliwa.
Katika kipindi cha kwanza kurushwa katika kituo hicho cha luninga siku moja baada ya uzinduzi wananchi wataanza kuangalia filamu iliyopewa jina la ‘Safari ya Nungwi’ iliyokusanya taarifa mbalimbali kuhusu tukio hilo la ajali lililoipata meli ya MV Spice Islander iliyozama katika kina cha bahari cha mita 350 wakati ikitoka Unguja kuelekea kisiwani Pemba Septemba 10 mwaka jana na kuacha msiba mkubwa kwa Taifa.
“Kwa kutumia filamu hii itakayokuwa ikirushwa hewani mara mbili kwa wiki tunajifunza kuwa wananchi wanahitaji kupewa elimu kuhusu usalama wao katika safari za majini; kabla, wakiwa safarini na baada ya safari, masuala ya bima na umuhimu wa kuweka fedha benki na ndio maana hata baadhi ya wadhamini wetu wanatoka katika sekta za fedha na bima,” anasema Bwana Masanja.
Aidha tunatoa shukrani kubwa kwa wadhamini wetu waliojitokeza na ambao wanaendelea kujitokeza leo napenda kuwataja baadhi yao kama Benki ya PBZ, Clouds Entertainment, Global Publishers, Asteri Insurance, Hamisi Pambakali na kampuni ya Azam Marine.Akizungumza Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya PBZ, Juma Hafidh alisema benki yao imeona umuhimu mkubwa wa kudhamini uzinduzi wa kipindi hicho kwani manufaa yake ni muhimu kwa jamii ambao ndio wateja wao.
“Kunapotokea mfano ajali waathirika wakubwa ndio wateja wetu tunaofanya nao biashara hivyo wananchi wakifahamishwa umuhimu mathalani wa kutosafiri na kiwango kikubwa cha fedha na kuweka benki pindi ikitokea misukosuko yoyote fedha zao zinakuwa katika mikono salama,” anasema mkurugenzi huyo wa masoko wa PBZ.
Uzinduzi wa kipindi cha luninga cha Mwana Dar es Salaam utakaofanyika katika Ukumbi wa kisasa wa Dar Live utapambwa na burudani mbalimbali na kuhusu nani atakuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo mtajulishwa katika taarifa tutakazokuwa tukiwatumia kabla ya tukio la uzinduzi.
MWISHO.
MWISHO.
0 Comments