Ramsey Nouah alipokuwa nchini kwa mualiko maalum wa swahiba wake Steven Charles Kanumba. 
 Ramsey Nouah (kushoto) akiwa na marehemu Kanumba.
Ramsey Nouah, akipozi na Lulu (kushoto).
Ramsey Tokumbo Nouah (kushoto) akiwa na Kajala Masanja.

APRILI mwaka jana msanii maarufu wa filamu kutoka nchini Nigeria, Ramsey Tokunbo Nouah alikuja Bongo kwa mualiko maalum wa swahiba wake ambaye kwa sasa ni marehemu, Steven Charles Kanumba.
Lengo la Ramsey kuja Bongo lilikuwa kushiriki katika filamu iliyopewa jina la Devil’s Kingdom ambayo iliandaliwa na Kanumba na kuwashirikisha wasanii wengine wa hapa nchini.
Kwa wasiojua, Ramsey na Kanumba walikuwa marafiki wakubwa sana hasa ikichukuliwa kwamba, kwa Nigeria Ramsey ni jina kubwa katika tasnia ya filamu kwani amejitanua kimataifa kama ilivyo Kanumba kwa hapa Tanzania.
Wakati leo nchi nzima bado imegubikwa na simanzi kufuatia kifo cha Kanumba, kuna mambo ambayo yatakuwa yakimshangaza Ramsey huko aliko.
Akiwa Tanzania, msanii huyo alipata fursa ya kukutana na wasanii wengine Bongo achilia mbali Kanumba na kufanya nao kazi kwa siku kadhaa.
Miongoni mwa wasanii ambao walibahatika kuwa karibu na Ramsey na kupiga picha pamoja ni Kajala Masanja ambaye leo hii yuko katika Gereza la Segerea akikabiliwa na kesi ya kutakatisha fedha haramu.
Mbali na Kajala, Elizabeth Michael (Lulu) pia alibahatika kupiga picha na Ramsey lakini leo hii naye anashikiliwa na polisi kwa madai ya kuhusika na kifo cha Kanumba.
Ukiacha hao, Kanumba pia alipiga picha nyingi na Ramsey lakini naye leo amepumzika katika nyumba ya milele.
Kwa maana hiyo, kama leo Ramsey atatua Bongo akitarajia kupokelewa na mmoja kati ya wasanii hao, hawezi kufanikiwa kwani wote wako matatizoni ukiachilia mbali Kanumba ambaye hawezi kumuona tena. Hicho ndicho kitakachomshangaza Ramsey.