Timu ya soka ya Real Madrid nchini Uhispania imetangaza kuwa imebadilisha nembo yake kwa ajli ya kuonyesha heshima kwa mashabiki wake wafuasi wa dini ya Kiislamu.

Tovuti ya Sonhaber imeripoti kuwa viongozi wa timu hiyo mashuhuri duniani ya mpira wa miguu wamesema kuwa ili kuweka wazi heshima kwa mashabiki Waislamu na kuvutia idadi kubwa zaidi ya mashabiki wengine, Real Madrid imebadilisha nembo yake ya msalaba ambayo imekuwa ikiitumia kwa kipindi cha karibu miaka mia moja.

Vyombo vya habari vya Uhispania vimeripoti kuwa, viongozi wa Real Madrid wameashiria idadi kubwa ya mashabiki Waislamu wa timu hiyo na kuchukua uamuzi wa kuondoa alama ya msalaba iliyokuwa sehemu ya juu ya nembo yake, kwa sababu alama hiyo ilikuwa ikisababisha utata na suitafahamu kati ya mashabiki.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa timu nyingine mashuhuri ya Uhispania Barcelona, pia ilichukua hatua kama hiyo na kuondoa alama ya msalaba katika nembo yake.