LEO ndio leo Arumeru Mashariki wananchi wanajitokeza kuanzia saa moja asubuhi kupiga kura kuchagua mbunge wao baada ya kukaa kwa zaidi ya siku 90 bila uwakilishi bungeni kutokana aliyekuwa mbunge wao, Jeremiah Sumari, kufariki dunia Januari.
Mpaka jana, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilishathibitisha kukamilika kwa maandalizi yote
ya uchaguzi huo mdogo, kazi iliyobaki ni leo wananchi kuwapigia kura wagombea wa vyama vinane vinavyoshiriki huku upinzani mkali na wa dhahiri ukionekana kati ya Sioi Sumari
wa CCM na Joshua Nassari wa Chadema.
Jana vyama vinavyoshiriki vilihitimisha mikutano yao ya kampeni, kila kimoja kwa staili yake.
CCM ikimtegemea Mwenyekiti wake mstaafu, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyeongoza timu ya chama hicho kufunga kampeni, kwa staili ya kuwagawa viongozi wake wa juu wakiwamo wabunge katika kata zote.
Utaratibu huo ni tofauti na ambao umekuwa ukitumiwa na chama hicho cha kumwalika kiongozi wake wa kitaifa kufungua na kufunga kampeni kwa mikutano mikubwa na hivyo kufanya wanachama na wafuasi wake wa vijiji na kata mbalimbali kukusanyika pamoja.
Jana tangu asubuhi, wabunge wa CCM, wajumbe wa Kamati Kuu, wajumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa, Jumuiya ya Wanawake (UWT), Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Umoja wa Wazazi na wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Arusha na wilaya ya Arumeru, waligawanyika katika
kata zote 17 za jimbo hilo lenye vijiji 74 ili kumwombea kura Sioi katika muda huo wa lala salama.
Baada ya kuhutubia mkutano wa kwanza wa kufunga kampeni katika kijiji cha Patandi, Tengeru
juzi jioni, jana Mkapa alifanya mkutano mwingine katika kijiji cha King’ori, ukihusisha WanaCCM wa kata hiyo na za jirani huku zingine zikiwa na mikutano yao pia.
Mbali na mkutano huo wa Mkapa, mikutano mingine ilihutubiwa na Katibu Mkuu, Willson
Mukama, Mjumbe wa Idara ya Itikadi na Uenezi Taifa, Nape Nnauye, Katibu wa Idara ya
Uchumi na Fedha Taifa, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde na viongozi wengine.
Chadema
Kwa upande wake, Chadema pamoja na kuwa na mkutano mkubwa wa kufunga kampeni
Patandi, Tengeru, pia ilifanya mkutano mkubwa Usa River, maeneo ambayo yanatajwa kuwa
ngome kubwa ya chama hicho kwa kuwa na wafuasi wengi.
Katika mikutano hiyo, Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu,
Dk. Willibrod Slaa na wabunge maarufu wa chama hicho walimnadi Nassari katika kipindi hicho cha lala salama.
Nassari alisema ana matumaini ya kuwa mbunge wa jimbo hilo na kuwaomba wananchi wamchague ili atatue kero za afya, maji, elimu na mengine, kwa kutumia fedha za Mfuko wa Jimbo na kuistawisha Arumeru Mashariki.
AFP, SAU
Mgombea wa AFP, Abdallah Mazengo, alisema kura ni siri ya mpiga kura, lakini yuko tayari
kwa ushindi, kwani anatambua matatizo ya wananchi hao na kuongeza kuwa akichaguliwa atahakikisha ardhi iliyochukuliwa na wenye fedha inarudi mikononi mwa wananchi.
Shaaban Kirita, wa SAU alisema akichaguliwa atahakikisha wananchi wanalima kisasa badala
ya kilimo cha msimu kinachotegemea mvua hivyo atahakikisha wananchi wanavuna maji ya
mvua, ambayo yatawezesha kulima mazao kila mwaka.
Wakati wagombea wakihitimisha kampeni zao, wananchi wamesema wameshasikia sera za
wagombea na kuzichuja, na wanachosubiri ni kura, huku wakisema watakubali matokeo na kuwa tayari kushirikiana na mbunge atakayeibuka mshindi.
Tume
Wakati huo huo, NEC imesisitiza wananchi kutotumia fomu namba 17 ambayo imetangazwa
kutumika na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kwa wananchi wasio na vitambulisho vya kupigia kura.
Aidha, tume hiyo imewasihi wapiga kura kuhakikisha wanakaa umbali wa meta 200 kutoka vituo vya kupigia kura na kutoa vipaumbele kwa wajawazito, walemavu, wananyonyeshao na
wenye mahitaji maalumu ili wasipange foleni kupiga kura.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, alipokuwa akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu upigaji kura unaofanyika leo.
Alisema fomu namba 17 itatumika pale Msimamizi wa Uchaguzi atakapomtilia shaka mpiga
kura na si kutumika kupiga kura na kusisitiza kuwa kitambulisho cha kupigia kura ndicho pekee kitakachomambuliwa.
Alisema: ”Baadhi ya viongozi wamekuwa wakiwaambia wananchi watumie fomu namba 17, lakini NEC tunasema fomu hiyo haitatumika bali kitambulisho cha mpigakura na vituo vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa 10 jioni na kama kuna watu muda wa kufunga utawakuta vituoni, Msimamizi wa Kituo atasimama mwisho ili watu hao wapige kura,” alisema.
Aliongeza kuwa, mawakala wa vyama vya siasa wana wajibu wa kulinda maslahi ya vyama vyao na wagombea, lakini hawatakiwi kuingilia masuala ya utendaji ambayo yamekabidhiwa kwa Msimamizi wa Kituo na endapo wataona hitilafu yoyote na kushindwa kupata maelekezo ya kutosha kutoka kwa msimamizi huyo wataeleza malalamiko yao kwa kutumia fomu namba 14 na fomu namba 17 zilizotolewa na Tume.
Aidha, alisema baada ya kupiga kura kumalizika matokeo yatajazwa kwenye fomu maalumu ambazo zitasainiwa na Msimamizi wa Kituo na wakala na matokeo yote yakishapokewa na Msimamizi kwa upande wa ubunge yatatangazwa na kwa upande wa udiwani yatatangazwa na Msimamizi Msaidizi.
Nje ya ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi, Trasias Kagenzi, vifaa vya kupigia kura vilikuwa
vikipakiwa kwenye magari na kupelekwa kwenye kata mbalimbali tayari kwa uchaguzi.
Polisi Naibu Kamishna wa Polisi ambaye ni Msimamizi wa Operesheni ya Uchaguzi, Isaya Mungulu, alisema kuna mwonekano wa wananchi kutotii sheria, hivyo alitoa angalizo kwa wananchi wanaopiga kura kukaa meta 200 mara wamalizapo kupiga kura.
Alisema Polisi haitavumilia fujo kwenye vituo na ushabiki wa vyama, bali itasimamia sheria, kanuni na taratibu, na endapo kutatokea fujo Polisi imejipanga kukabiliana nazo. |
0 Comments