MSANII wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’, amemwaga chozi mahakamani baada ya kubanwa na askari Magereza waliokuwa wakimlinda akipitishwa katikati ya kundi la watu waliofurika mahakamani kusikiliza kesi hiyo ya mauaji inayomkabili.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana ilifurika watu wakiwemo waandishi wa habari huku wapigapicha wakijitahidi kupata picha ya msanii huyo baada ya siku ya kwanza ya kesi hiyo kushindwa kupata picha hiyo. Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Rita Tarimo ilikuja kutajwa.

Baada ya kuingia mahakamani huku akilia, kimya kilitawala mahakamani hapo kwa muda huku askari wakijaribu kumtuliza.



Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda aliiomba Mahakama kuondoa watu wote kwa hofu ya kusababisha vurugu mahakamani hapo.

Kutokana na ombi hilo, Hakimu Tarimo aliamuru watu waliojazana katika chumba hicho kuondoka kabla mshitakiwa hajaondolewa ili kurudishwa mahabusu.

<><> <><>
Lulu alifikishwa mahakamani hapo na gari la Polisi aina ya Toyota Hiace akiwa mshitakiwa peke yake huku akilindwa na askari Magereza.

Baada ya kutajwa kwa kesi yake saa tano asubuhi, Lulu aliondolewa haraka mahakamani hapo akitumia gari hilo hilo huku likipiga ving’ora.

Kamishna Haki za Binadamu amtetea Wakili wa kujitegemea, Kennedy Fungamtama, ambaye anamtetea Lulu, aliwatambulisha mawakili wenzake wa utetezi katika kesi hiyo akiwemo Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu, Joaquine De-Mello, Peter Kibatala na Fulgence Masawe.

Kaganda alidai kuwa kesi ilifika mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Aliiomba Mahakama kupanga siku nyingine ya kutaja na ikapangwa Mei 7. Lulu anadaiwa kumwua msanii mwenzake, Kanumba Aprili 7, Sinza Vatican, Dar es Salaam. Yuko mahabusu kwa sababu kesi ya mauaji haina dhamana.