MBUNGE mteule wa Arumeru Mashariki mkoani Arusha, Joshua Nassari,(pichani) amemshukuru Mungu kwa kumwezesha kuwa na maono ya kuwa mbunge na kukishukuru chama chake na wapiga kura kwa kumchagua.

Nassari ambaye alikuwa mgombea wa Chadema, alisema hayo jana muda mfupi baada ya kukabidhiwa hati na kutambuliwa rasmi kuwa mbunge mteule wa jimbo hilo, kwa kushinda uchaguzi mdogo uliofanyika juzi.

“Tulianza na Mungu na tumemaliza na Mungu…si tu kwa kura peke yake, bali tutafanya hivyo hata kwa masuala ya maendeleo pia,” alisema Nassari ambaye katika uchaguzi huo, aliwashinda wagombea wenzake saba akiwamo mshindani wake wa karibu, Sioi Sumari wa CCM.

Mbunge huyo mteule ambaye ataapishwa Aprili 10 Dodoma, aliwashukuru pia polisi kwa kufanya kazi kubwa ya kusimamia ulinzi wakati wote wa kampeni na wakati wa upigaji kura.

Hata hivyo, alimwomba Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arumeru, kuwaachia huru wapenzi wa chama hicho waliokamatwa usiku wa kuamkia jana, kwa madai ya kufanya fujo na mikusanyiko.
Alisema angependa kusherehekea ushindi wake akiwa nao. Aliahidi kuwa vipaumbele atakavyozingatia katika kipindi chake ni kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya ardhi, maji, elimu na kuanzisha Mfuko wa Maendeleo wa Vijana na Wajane.

Aidha, alisema leo ataanza kazi rasmi kwa kuchimba visima viwili vya maji katika Kata ya Mororoni. Aliwahamasisha wafuasi hao kujitokeza kwa wingi kufanya kazi hiyo ambayo tayari amekwishapewa fedha kwa ajili hiyo kutoka kwa Mbunge wa Moshi Vijijini, Philemon Ndesamburo (Chadema).



Matokeo yalivyokuwa Nassari aliibuka mshindi baada ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Trasias Kagenzi, kumtangaza kuwa amepata kura 32,972 kati ya 60,699 zilizopigwa, hivyo kumrithi Jeremiah Sumari wa CCM aliyefariki dunia Januari 19 kutokana na saratani ya ubongo.

Kagenzi alisema Sumari alijizolea kura 26,752, wakati wagombea wengine, Abdallah Mazengo wa AFP akipata kura 139, Mohamed Mohamed wa DP kura 77, Hamis Kiemi wa NRA kura 35, Shabani Kirita wa SAU kura 22, Chipaka Moova wa TLP kura 18 na Charles Msuya wa UPDP kura 18.

Kagenzi alisema idadi ya kura halali zilikuwa 60,038 na kura zilizoharibika zilikuwa 661 na kuongeza kuwa watu 127, 455 walijiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Wakati Kagenzi akitangaza matokeo hayo, wanachama wa Chadema ambao walikesha kwenye ofisi hizo kusubiri matokeo, walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali huku wakisema “Freedom is Coming (Ukombozi Unakuja) na People’s Power (Nguvu ya Umma)” na wengine wakicheza kushangilia matokeo hayo kwa kusema “CCM bye bye (CCM kwa heri)”.

Awali mbwembwe zilianza usiku wa kuamkia jana, baada ya maelfu ya wakazi wa maeneo hayo na yale jirani ya Arusha Mjini na Kilimanjaro kuonekana kwa wingi kuanzia saa 12 jioni baada ya kuanza kupata matokeo ya awali yaliyoonesha kuwa kwenye vituo vingi mgombea wao anaongoza.

Katika ukumbi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Usa River, ambako ndiko majumuisho ya kura yalifanyika, viongozi na wapambe wa CCM hawakuonekana isipokuwa mawakala wao.

Badala yake, eneo hilo lilikuwa na wapenzi wengi na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Chadema akiwamo Mwenyekiti, Freeman Mbowe na wabunge.

Ilipofika saa sita usiku, Sioi aliingia katika viwanja vya ofisi hizo ambavyo vilikuwa vimejaa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU). Baada ya kuingia kwenye ukumbi, ghafla salamu ya “People’s…” zilihanikizwa na kuitikiwa na wanachama wao kwa sauti kubwa ya “Power!”.

Sioi ambaye alionekana kukosa furaha, hakukaa ndani ya ukumbi huo kwa muda mrefu na alitoka nje mara kadhaa kabla ya kutoka kabisa saa 10 alfajiri na hakurudi tena. Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, baada ya kumtangaza Nassari kuwa mshindi, alimkabidhi hati ambayo hata hivyo, si Sioi wala wakala wake walioisaini.

Wagombea wengine wa vyama vya NRA, TLP na UPDP nao pia hawakuisaini. Pamoja na hayo Sioi alisema amekubaliana na matokeo kwani katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa.

Imeandikwa na Veronica Mheta, Arumeru na Halima Mlacha, Dar