Mgombea urais kwa tiketi ya chama cha kisoshalisti nchini Ufaransa Francois Hollande, ameshinda duru ya kwanza ya uchaguzi nchini humo.

Kura nyingi zikiwa zimehesabiwa Bw Hollande tayari amepata asilimia 28 ya kura.
Nicolas Sarkozy anafuatia kwa asilimia 27 hii ikiwa ni idadi ndogo zaidi kwa rais yoyote wa taifa hilo ambaye amewahi kugombea tena kiti hicho.

Haijawahi kutokea kuwa rais aliyemadarakani anashindwa kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi.

Na matokeo haya yanampa mpinzani wa Rais Sarkorzy, Francois Hollande nafasi nzuri sana katika duru ya pili ya uchaguzi huo utakaofanyika baada ya wiki mbili.

Hata hivyo kilicho washangaza wengi baada ya matokeo hayo kutangazwa ni idadi ya kura chama kinacho egemea upande wa kulia kilipata.

Kwa makadirio tu, mtu mmoja kati ya wapiga kura watano nchini Ufaransa alikipigia kura chama hicho, hii ikiwa idadi kubwa zaidi ya kura chama hicho cha Front Nationale kilicho pata kwenye uchaguzi wowote nchini humo.

Rais Sarkorzy anasema matokeo hayo yanaonyesha hali ya wasi wasi raia wa nchi hiyo wanayo na ni kura ya maoni dhidi ya utawala wake.

Hata hivyo ametoa changamoto kwa mpinzani wake ajitokeze kwenye mdahalo kati yao kabla duru ya pili ya uchaguzi huo.

Lakini bila shaka kutokana na uchache wa kura alizopata dhidi ya Rais Sarkorzy, kiongozi huyo wa chama cha kisoshalisti, Francoise Hollande atakuwa makini sana asipoteze kura muhimu.


Bw Hollande anasema wafaransa wanaimani na mradi wake kwa nchi hiyo ambao umelenga kurejesha haki, usimamizi bora wa uchumi wa nchi, ukuzaji wa nafasi za kazi, kulinda viwanda na kujiandaa vyema kwa siku za usoni.