Filbert Rweyemamu,
 Arusha
MAKAMU wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaelimisha wataalamu zaidi na kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya utafiti ili kupunguza vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano na wajawazito nchini.

Akifungua mkutano wa 26 wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini(NIMR), Dk Bilal alisema kuwa utafiti ni njia kuu ya kutambua tatizo na namna ya kukabiliana na vifo hasa vinavyotokana na magonjwa ya kuambikiza.

“Suala la afya linaingiliana na malengo mengine ya millenia mbayo ni umasikini na njaa, elimu, jinsia sayansi na teknolojia. Maji na mazingira ili kufikia malengo haya rasilimali za nje na ndani zinatakiwa kwa sababu changamoto hii inahitaji uwekezaji mkubwa,”alisema Dk Bilal.
Alisema kwa Tanzania ili kufikia malengo ya Milenia,Serikali iliamua kutafsiri mpango huo katika dhana Mpango wa Kupunguza na Kuondoa Umaskini(Mkukuta).

Makamu wa rais alisema kuwa hadi sasa imepita miaka 12 tangu mpango huo uanze na bado Tanzania ina idadi kubwa ya watu maskini huku watoto na wanawake wakifariki dunia kwa kukosa huduma za afya huku watu wengi wakikabiliwa na changamoto ya magonjwa yanayoambukiza na yasiyo ya kuambukizwa.


Alisema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine Kusini mwa Jangwa la Sahara zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa umaskini unaosababisha huduma zisizofaa za afya kutokana na huduma muhimu kutowafikia walengwa kwa wakati.

Naye Mkurugenzi mkuu wa NIMR, Dk Mwele Malicela alisema kuwa pamoja na maendeleo mazuri yaliyofikiwa katika kukabiliana na vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano vinatokana na ugonjwa wa Malaria, taasisi hiyo bado inawajibu wa kufanyia kazi matokeo ya tafiti wanazozifanya katika vituo vyote nchini.

Kongamano hilo linalenga kuwashirikisha watafiti,watunga sera na wadau wa afya duniani ili kubadilishana uzoefu katika Nyanja mbalimbali za kisayansi.