Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk Wilbrod Slaa, amesema hayupo tayari kula sahani moja na watuhumiwa wa ufisadi watakaojiunga na chama hicho.
Amesema Chadema ipo makini katika kuwapokea wanachama na viongozi wanaotoka CCM, lakini haitakuwa rahisi kukigeuza chama hicho kuwa pango la mafisadi.
Alisema hayo wakati akimpokea aliyekuwa diwani wa kata ya Lugata katika wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza (CCM), Adrian Tizeba.
Tizeda alikihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Baada ya kutangaza kujiengua CCM, Tizeba alikabidhiwa kadi ya Chadema na Dk.Slaa ambaye alisema kwamba hiyo ni zawadi kutoka kwa Mungu baada ya kuwa wamemvua uanachama diwani wa Katoro kupitia chama hicho, aliyemtaja kwa jina moja la Gervas.
Akihutubia mkutano huo wa hadhara, Dk.Slaa alisema kwamba Chadema kiko makini katika kupokea wanachama kutoka CCM na kamwe hakitakubali kupokea mafisadi.
“Yapo maneno yanasemwa kuhusu wanaCCM kuhamia Chadema, lakini nataka niwaambie kwamba tuko makini, mimi Dk.Slaa siwezi kula sahani moja na mafisadi lazima tunajiridhisha kwanza kabla ya kumpokea mtu”alisema.
Tizeba anakuwa diwani wa tatu katika kipindi cha siku tatu kujiengua kutoka CCM na kujiunga na Chadema.
Siku tatu zilizopita aliyekuwa Diwani wa Kata ya Sombetini mkoani Arusha, Alphonce Mawazo alitangaza kukihama CCM, na juzi diwani wa kata ya Nyampulukano wilaya ya Sengerema, Hamisi Magwao alifuata nyayo hizo.
Tizeba ambaye ni kaka mkubwa wa Mbunge wa Buchosa, Dk.Charles Tizeba, alitangaza uamuzi wa kujiengua CCM jana jioni katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini hapa na kuhutubiwa na Katibu Mkuu wa Chadema Dk.Wilbroad Slaa na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.
Akitangaza kukihama CCM, Tizeba alisema amechoshwa na tabia za viongozi wa chama hicho, kushindwa kushughulikia matatizo ya msingi yanayowakabili wananchi.
Katika hatua nyingine, Dk.Slaa alitangaza azma ya chama chake kumshughulikia kisheria Mkuu wa Mkoa mpya wa Geita, Said Magalula, ambaye anadaiwa kushirikiana na wawekezaji wa mgodi wa GGM kuwanyanyasa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwafyatulia risasi.
Alisema kwamba kama Mkuu huyo wa mkoa anataka kuwa salama katika mkoa wa Geita, hana budi kuwalinda wananchi dhidi ya wawekezaji wanaonyanyasa raia bila sababu za msingi.
Naye Lema alitumia mkutano huo kuzungumzia hukumu iliyotengua ushindi wake wa ubunge katika jimbo la Arusha Mjini akisema kuwa alihukumiwa kihuni.
Hata hivyo alidai kuwa kimsingi hukumu hiyo haijampunguzia chochote kwa sababu anaamini yeye bado ni Mbunge, isipokuwa amepumzishwa kwa muda tu na baadaye atarejea katika nafasi yake hiyo.
Kwa upande mwingine, wanachama 83 wa CCM tawi la Igalagalilo kata ya Kasungamile wilayani Sengerema walijiengua kutoka chama hicho na kujiunga Chadema.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya diwani wa kata ya Nyampulukano Hamis Mwagao, kukihama CCM na kutangaza kujiunga Chadema.
Katibu wa Chadema jimbo la Sengerema ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana (Taifa), Rafiki Rufunga alisema jinamizi la watu kujiunga na Chadema linatokana na serikali kushindwa kutatua kero zinazowakabili wananchi na ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo.
Alisema wananchama wa CCM tawi la Igalagalilo walijiunga Chadema April 13, mwaka huu wakati wa kurudisha fomu ya mgombea wa chama hicho katika uchaguzi mdogo wa mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho.
Miongoni mwa wanachama hao yumo Katibu wa Shina (balozi) Kusekwa Masheku na kamanda wa sungusungu Hamisi Nteminyanda.
0 Comments