WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema kesho atatoa tamko la Serikali juu ya habari za kuwapo mawaziri ambao wamelazimishwa kujiuzulu na wakakubali.
Pinda alitoa kauli hiyo jana baada ya kuulizwa na waandishi wa habari juu ya msimamo wake kuhusu habari zilizoandikwa na baadhi ya magazeti jana kuwa mawaziri wanane wamekubali kujiuzulu kwa kuandika barua baada ya kutakiwa kufanya hivyo na wabunge wa CCM.
Kikao cha wabunge wa CCM kilifanyika Alhamisi na juzi baada ya wenyeviti wa kamati zinazosimamia Serikali katika masuala ya fedha kuwasilisha taarifa zao zilizoibua tuhuma za ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma ndani ya Serikali.
Pinda ambaye juzi usiku alitajwa na Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama kuwa angezungumzia kwa kina masuala yaliyojiri ndani ya kikao cha wabunge wa CCM, hakufanya hivyo hali iliyowalazimisha waandishi wa habari kumvizia kabla hajaondoka kwenye Viwanja vya Bunge.
Viongozi wa kikao hicho waliitisha mkutano wa wanahabari juzi kuwaeleza masuala hayo, lakini ghafla Mhagama akajitokeza na kueleza kuwa wamelazimika kumwachia suala hilo Waziri Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM ili aweze kulizungumzia suala hilo.
Lakini tofauti na ahadi ya Mhagama, Pinda alionekana kutokuwa tayari kuzungumzia suala hilo, hali iliyowalazimu waandishi wa habari wamfuate kabla ya kuondoka Viwanja vya Bunge aeleze msimamo wa Serikali juu ya kilichoandikwa na magazeti.
“Mimi sijasoma hayo magazeti, mnataka nizungumze nini?” Alihoji Pinda na kuambiwa na waandishi hao kuwa ni juu ya kujiuzulu kwa baadhi ya mawaziri, lakini akahoji tena: “Inategemea hizo habari mmezitoa wapi.”
Waandishi walimjibu kuwa walielezwa na Mhagama kuwa angezungumzia suala hilo leo (jana), lakini hawakuona dalili za kuitishwa kwa mkutano huo, hivyo wakataka atoe kauli juu ya habari hizo.
Baada ya kauli hiyo kutoka kwa wanahabari ndipo Pinda akasema: “Habari kamili ni Jumatatu, vuteni subira,” alisema Pinda na kuingia kwenye gari lake akaondoka kwenye Viwanja ya Bunge. Hadi juzi usiku, kulikuwa na tetesi za mawaziri wanane kukubali kujiuzulu baada ya kushinikizwa na wabunge.
Tetesi hizo zilieleza kuwa mawaziri hao waliandika barua za kujiuzulu na siku ya mwisho ya kuwasilisha barua hizo ni Jumatatu.
Habari zilidai kuwa mawaziri hao waliitwa mmoja mmoja juzi jioni kabla ya kikao cha wabunge wa CCM. Taarifa za mawaziri hao zilivuja kwa wanahabari na baadaye mjumbe wa Sekretarieti wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Januari Makamba, akaita wanahabari saa nne usiku ili kuzungumzia suala hilo.
Wanahabari wakiwa na hamu ya kuelezwa kilichojiri ndani ya kikao hicho, baadaye Mhagama akajitokeza na kueleza kuwa suala hilo angelizungumzia Mwenyekiti wao, Pinda.
Mmoja wa mawaziri anayetajwa kutakiwa kujiuzulu ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo ambaye wakati wa mjadala bungeni, baada ya taarifa kuwasilishwa na kamati zinazoisimamia Serikali, alituhumiwa na wabunge wengi kuwa si mwadilifu na anaongoza kwa kutumia fedha za umma.
Mkulo pia alituhumiwa kuuza mali za Serikali kiholela bila kushirikisha Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC). Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka uliopita wa fedha ilitoa mifano ya viwanja vilivyouzwa na Mkulo bila kushirikisha CHC.
Waziri mwingine aliyetajwa kujiuzulu ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, ambaye wizara yake inatuhumiwa kutumia Sh bilioni moja kwenye maonesho ya Nanenane. Mwingine ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu ambao wanatuhumiwa kumlinda Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango (TBS).
Kwenye orodha hiyo yumo pia Waziri wa Kilimo na Ushirika Jumanne Maghembe anayeelezwa kushindwa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watendaji wa Bodi ya Pamba ambao ‘walitafuna’ Sh bilioni 2 zilizotolewa na Serikali kulipa wakulima wa zao hilo baada ya kutokea matatizo ya uchumi. Pia Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ambaye wizara yake ilitajwa na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa imegubikwa na rushwa katika ununuzi wa mafuta ya kuzalisha umeme wa dharura.
Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika, naye yumo kwa wizara yake kuonesha kufanya ‘madudu’ kutokana na ulaji uliokithiri kwenye halmashauri za wilaya. Waziri huyo anashutumiwa kushindwa kuchukua hatua kwa watendaji wa chini yake na badala yake amekuwa anawahamisha vituo vya kazi wabadhirifu hao.
Habari hizo pia zilimtaja Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, ambaye wizara yake inatuhumiwa kwa mauaji ya tembo wengi mwaka jana kuliko wakati wowote ule. Pia kuwapo na utata katika ugawaji vitalu vya kuwindia. Wabunge wagawanyika Wakati hilo likitokea, jana wabunge waligawanyika kuhusu masuala nyeti kwa Taifa yanayosababisha kupotea kwa rasilimali za nchi.
Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), alisema kubadilisha mawaziri hakuwezi kuleta suluhu ya muda mrefu ya matatizo yanayoikabili nchi katika sekta tofauti iwapo mfumo wa utawala hautabadilishwa kwa kuidhibiti Serikali Kuu katika kuhodhi madaraka.
Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alipenyeza sera ya majimbo inayotumiwa na chama chake wakati akichangia taarifa ya Kamati za Kisekta za Bunge, zilizoonesha kwamba yapo matatizo makubwa katika maeneo mbalimbali. “Utalaumu mawaziri, utalaumu Serikali, utalaumu wakurugenzi au kila mtu mwenye mamlaka ya kiutendaji, lakini mayai yote unayalundika katika kapu moja, una waziri mmoja anasimamia mafuta, madini, gesi, lazima awe na uwezo wa ajabu,” alisema Mbowe.
Alisema tatizo lililopo ni madaraka kulundikwa kwa mawaziri licha ya nchi kuwa kubwa. Alisisitiza, “mawaziri kwa kweli wanazidiwa. Utakavyobadilisha mawaziri kwa vyovyote kama mfumo wa utawala hautabadilishwa, tatizo litabaki palepale.
“Tuanzishe utaratibu wa kuwa na serikali za majimbo. Bahati mbaya watu wanafikiri hizi ni sera za ubaguzi au za kikabila,” alisema na kusisitiza kwamba itaondoa hatari ya kulundika madaraka kwa mtu mmoja ambacho ndicho chanzo cha matatizo.
Alipendekeza Katiba mpya, ielezwe ni namna gani raslimali za nchi zitasaidia kuleta manufaa kwa kuangalia ni namna gani madaraka yanagawanywa. Alisema haiwezekani madaraka yote yawe Dar es Salaam na si nchi kuendelea kuwekwa katika kapu moja la mayai huku waziri mmoja akiwajibika kwa nchi nzima.
Alishauri vyama vyote vya siasa na dini kutafakari juu ya sera hiyo, huku akisisitiza kwamba kuondoa mawaziri na kuingiza wengine ingawa kunaweza kuongeza ufanisi kwa kiasi fulani, lakini ni suluhu ya muda mfupi.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano, Sera na Uratibu), Stephen Wasira kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe alisema nchi si kubwa kiasi cha kuhitaji serikali nyingi. Alisema Kenya wamejaribu mfumo huo lakini sasa wanalalamika, kwamba ni ghali.
“Tukiimarisha miundombinu ya barabara na mawasiliano na simu, Tanzania itakuwa nchi ndogo kama dunia inavyokuwa ndogo kwa sababu ya mawasiliano. Hoja si kuongeza wabunge, Bunge lenyewe moja linatushinda kulipa posho, tukiweka 30 tutalipanaje?” Alihoji Wasira.
Akichangia kuhusu mfumuko wa bei, kupanda kwa gharama za maisha na hali tete ya uchumi yakiwamo matumizi ya Serikali kuwa makubwa kuliko mapato, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alisema tatizo lililopo ni uwajibikaji duni. Alishauri mawaziri wanaojiuzulu wasiachwe hivi hivi bali wawajibishwe kwa matatizo waliyoyasababisha ili liwe fundisho kwa wengine watakaoshika nafasi hizo. Alitoa mfano kwamba mwaka 2008, hali ilikuwa tete kama ilivyo sasa na iwapo mawaziri waliowajibika wakati ule wangechukuliwa hatua, hali isingejirudia.
“Mwaka 2008 Taifa lilikuwa katika hali kama hii. Lakini kwa kuwa tuna kawaida ya kuchukua hatua nusunusu, leo hii tunarudi tena kujadili. Watu wanaomshauri Rais wachukue jambo hili. Pamoja na mawaziri kujiuzulu, achukue hatua za ziada.
Mawaziri wa 2008 wangechukuliwa hatua hali hii isingejirudia. Rais akitumia mamlaka ya kikatiba ana uwezo wa kusafisha. Aidha, Mbunge huyo wa Ubungo ameshauri ukaguzi maalumu ufanyike kuhusu matumizi ya vyakula kutoka kwenye maghala ya Taifa na msamaha wa kodi kwenye vyakula vinavyoingizwa ndani kutokana na alichosema kuna ufisadi kutokana na misamaha hiyo kutoleta nafuu katika bei ya vyakula kwenye soko hususan Dar es Salaam. Pia alishauri CAG afanye ukaguzi maalumu kwenye akaunti ya deni la Taifa, ili kujua sababu za kuongezeka. Mbunge wa Mjimkongwe, Muhammad Ibrahim Sanya (CUF) aliwatuhumu mawaziri kuwa wamebaki kusafiri mara kwa mara nje ya nchi. “Mawaziri tulio nao wamebaki kuwa kama Vasco da Gama kazi yao kusafiri. Waziri aliyewekwa kusafiri hizo nchi ni mmoja tu, Membe (Bernard-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa),” alisema na kutoa mfano kwamba mwaka jana kuna kipindi mawaziri saba walikuwa nje kwa wakati mmoja. “Ukiwauliza wanarudi na nini zaidi, atakwambia amerudi na marashi ya mama watoto,” alisema. Kauli hiyo ya wabunge ilikuja huku kukiwa na shinikizo la kutaka mawaziri wajiuzulu hali iliyosababisha juzi kuanza mchakato wa kukusanya saini 70 kwa ajili ya kupeleka hoja ya kumwajibisha Waziri Mkuu wakidai ameshindwa kuwawajibisha mawaziri wake. Imeandikwa na Shadrack Sagati na Stella Nyemenohi, Dodoma.
0 Comments